Slot aambiwa anase watatu

Muktasari:
- Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, Keane alisema kocha Arne Slot hana namna nyingine zaidi ya kuongeza mastaa kadhaa kwenye kikosi chake kama anataka kurudi msimu ujao akiwa na nguvu na uwezo wa kutetea ubingwa.
LIVERPOOL, ENGLAND: GWIJI wa Ligi Kuu England, Roy Keane amesema Liverpool inahitaji kufanya usajili wa wachezaji watatu kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kama watahitaji kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu England msimu ujao.
Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, Keane alisema kocha Arne Slot hana namna nyingine zaidi ya kuongeza mastaa kadhaa kwenye kikosi chake kama anataka kurudi msimu ujao akiwa na nguvu na uwezo wa kutetea ubingwa.
Liverpool ilikumbana na kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Chelsea, Jumapili iliyopita na ilikuwa mechi yao ya kwanza tangu iliponyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.
Kiungo Enzo Fernandez aliifungia bao la kuongoza The Blues, kabla ya Chelsea kupata faida nyingine ya Jarell Quansah kujifunga. Virgil van Dijk aliifungia bao la kujifariji Liverpool, kabla ya Cole Palmer kufunga kwa mkwaju wa penalti kwenye dakika za mwisho kuipa timu hiyo inayonolewa na kocha Enzo Maresca pointi tatu muhimu kwenye msako wao wa kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Liverpool imefanya jambo muhimu kwenye usajili kwa siku za karibuni baada ya kuwasainisha mikataba mipya Van Dijk na Mohamed Salah. Lakini, wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa Juni 1, mkurugenzi wa michezo wa Liverpool, Richard Hughes atakuwa na kazi nzito kufanya usajili. Keane alitazama mechi hiyo ya Stamford Bridge na kufichua Liverpool imeshinda ubingwa wa ligi, lakini bado inahitaji kufanya maboresho kwenye baadhi ya maeneo.
Andy Robertson na Ibrahima Konate hawakucheza kwenye mechi hiyo, lakini Slot, ambaye aliwachezesha Kostas Tsimikas na Quansah, walionekana kuwa na kiwango duni kulingana na Keane.
“Wanahitaji kuwa na watu,” alisema Keane alipoulizwa kuhusu usajili.
“Hiyo ni changamoto kubwa inayowakabili Liverpool. Wanahitaji beki wa kushoto, beki wa kati na straika. Wameshinda ubingwa wa ligi, hilo litawasaidia kuwavutia wachezaji wengi. Kushinda ubingwa ni kitu kizuri, hivyo utalazimika kurudi kwa nguvu msimu ujao.”
Tsimikas na Darwin Nunez ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuuzwa wakati, Trent Alexander-Arnold atatimkia zake Real Madrid mwisho wa msimu. Liverpool inahitaji pia wasaidizi wa Ryan Gravenberch na Alexis Mac Allister.