Mbappe anataka kuikacha Ufaransa
Muktasari:
- Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa ameripotiwa kuwa aliwasiliana na Deschamps siku tatu kabla ya kikosi kuitwa na akamweleza kwamba hivi sasa yupo tayari kukitumikia, lakini kocha huyo aliamua kutomuita na alipoulizwa akasema anafikiria amefanya uamuzi bora kwa sasa.
PARIS, UFARANSA: BAADA ya kuripotiwa ameachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kitakachocheza michezo ya Uefa Nations League dhidi ya Israel na Italia, staa wa Real Madrid, Kylian Mbappe anadaiwa hataki tena kuichezea nchi hiyo ikiwa kocha ataendelea kuwa Didier Deschamps.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa ameripotiwa kuwa aliwasiliana na Deschamps siku tatu kabla ya kikosi kuitwa na akamweleza kwamba hivi sasa yupo tayari kukitumikia, lakini kocha huyo aliamua kutomuita na alipoulizwa akasema anafikiria amefanya uamuzi bora kwa sasa.
Taarifa za gazeti la Ufaransa la RMC zimefichua kuwa Mbappe ambaye alipewa taarifa na kocha huyo kabla kwamba hatamjumuisha katika kikosi, alimshukuru kwa uamuzi huo, lakini hajakubaliana naye na anachukulia kuwa ni dharau dhidi yake.
Mwandishi wa habari wa Ufaransa, Romain Molina amefichua kuwa staa huyo ana kinyongo na maelewano kati yake na kocha si mazuri, hivyo amepanga kutoitumikia tena Ufaransa chini ya Deschamps, vinginevyo matatizo baina yao yatatuliwe.
Mbappe ambaye alijiunga na Real Madrid katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu, hajawa na wakati mzuri katika kikosi hicho na tangu kuanza kwa msimu huu amefunga mabao sita katika mechi 10 za Ligi Kuu Hispania na asilimia 50 ya mabao hayo yametokana na penalti.
Inaelezwa Deschamps alikerwa na kitendo cha nyota huyo kuomba kutojumuishwa katika kikosi cha Ufaransa kilichocheza mechi za Uefa Nations League dhidi ya Israel na Ubelgiji.