Mazraoui kuwavaa Liverpool, Martinez mwezi ujao
Muktasari:
- Man United itakipiga na mahasimu wao Liverpool wikiendi hii, ambayo itajaribu kusaka ushindi wao wa kwanza baada ya kutokea kwenye vichapo vitatu mfululizo kutoka kwa Galatasaray, Crystal Palace na Chelsea. Lakini, Man United itapata mzuka kutokana na kurejea kwa beki wake mahiri, Noussair Mazraoui.
MANCHESTER, ENGLAND: TATIZO la majeruhi kwenye kikosi cha Manchester United bado linamsumbua kocha Ruben Amorim huku likimtishia kwenye upangaji wa timu yake kwenye mechi.
Man United itakipiga na mahasimu wao Liverpool wikiendi hii, ambayo itajaribu kusaka ushindi wao wa kwanza baada ya kutokea kwenye vichapo vitatu mfululizo kutoka kwa Galatasaray, Crystal Palace na Chelsea. Lakini, Man United itapata mzuka kutokana na kurejea kwa beki wake mahiri, Noussair Mazraoui.
Ripoti zinafichua wing-back huyo atakuwa fiti kutumika kwenye mechi dhidi ya Liverpool kama hatakuwa na tatizo lolote jipya litatokea kutoka sasa kumrudisha kwenye shida ya kukaa benchi ambayo imemfanya acheze mechi tatu tu msimu huu.
Mchezaji wa Man United, ambaye hatazamiwi kurejea uwanjani wikiendi hii ni beki wa kati, Lisandro Martinez, ambaye bado anauguza majeraha ya kufanyiwa upasuaji wa goti baada ya kuumia kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace, Februari 2025.
Awali, iliripotiwa beki huyo Muargentina angerejea uwanjani mwezi huu, lakini sasa, matarajio makubwa ni mwezi ujao wa Novemba licha ya kuanza kufanya mazoezi ya mpira mwezi uliopita. Kocha Amorim hataki kumharakisha mchezaji huyo akiwa na hofu ya kumfanya aumie tena kama atakuwa amepona na kuwa fiti kwa asilimia 100.