Mavumba ya Carrick kwa Mbeumo sio poa
Muktasari:
- Carrick ameanza kazi Man United kwa mafanikio makubwa, akishinda mechi zake mbili za mwanzo dhidi ya Manchester City na Arsenal.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Michael Carrick amevuruga mipango iliyowahi kuwekwa na kocha wa zamani wa timu hiyo Ruben Amorim kuhusu mshambuliaji Bryan Mbeumo siku chache tu baada ya kuajiriwa.
Carrick ameanza kazi Man United kwa mafanikio makubwa, akishinda mechi zake mbili za mwanzo dhidi ya Manchester City na Arsenal.
Vilevile moja ya mafanikio makubwa chini yake imekuwa ni kiwango bora cha mchezaji aliyesajiliwa katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, Mbeumo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon alifunga mabao dhidi ya City na Arsenal na kufikisha jumla ya mabao tisa katika mashindano yote msimu huu tangu alipotua Old Tafford akitokea Brentford.
Licha ya ukweli kiwango chake hakijabadilika sana tangu Carrick achukue nafasi ya ukocha, lakini kunaonekana kuna mabadiliko kidogo.
Kwa mujibu wa ESPN, kocha wa zamani Amorim alikuwa akimtumia Mbeumo kucheza nafasi tofauti maeneo mbalimbali ya safu ya ushambuliaji, lakini Carrick anaonekana kupendelea zaidi kumchezesha kama mshambuliaji wa kati na anampa uhuru wa kusogea maeneo mbalimbali uwanjani.
Amad na Patrick Dorgu wamepangwa kumsaidia kutoka pande zote mbili za uwanja (kulia na kushoto), huku Bruno Fernandes akicheza nyuma yake kama mtoaji wa pasi za mwisho.
Hata hivyo, mpango huo unaweza kuhitaji marekebisho kidogo baada ya Dorgu kuumia katika mechi dhidi ya Arsenal na kutarajiwa kukaa nje kwa muda mrefu.
Alipoulizwa mapema mwezi huu kitu gani kimebadilika tangi Carrick achukue mikoba, Mbeumo alisema: "Kila kitu kimebadilika kwa kiasi fulani. Mazoezi ni tofauti, mtazamo ni tofauti. Tunajua tuna lengo moja tu na mwelekeo mmoja, hivyo tunapaswa kufanya kila kitu ili kulitimiza. Kila kocha ana tabia yake na njia yake ya kufanya kazi na kocha huyu anaifahamu klabu vizuri sana."
Nyota wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Petit, hivi karibuni alimsifu sana Mbeumo kwa kiwango chake: "Ni mchezaji mwenye akili sana. Ana ubunifu mkubwa mbele ya lango. Pia ni mzuri sana katika kutoa pasi za mabao. Napenda sana anavyopambana. Anaongeza kitu tofauti katika safu ya ushambuliaji. Si mchezaji wa nguvu sana kimwili, lakini anatoa kila alichonacho uwanjani."