Maumivu makubwa! Afcon 2021 yatikisa vigogo Ligi Kuu England

Muktasari:

MAUMIVU. Arsenal haitakuwa na huduma ya mastaa wake wanne kwa mwezi Januari, mwakani wakati michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakapokuwa na madhara makubwa kwenye Ligi Kuu England.

LONDON, ENGLAND. MAUMIVU. Arsenal haitakuwa na huduma ya mastaa wake wanne kwa mwezi Januari, mwakani wakati michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakapokuwa na madhara makubwa kwenye Ligi Kuu England.

Arsenal ina orodha ya mastaa kadhaa muhimu kabisa kwenye kikosi chao ambao watakwenda kucheza michuano hiyo ya kimataifa, ambayo itafanyika kati ya Januari 9 na Februari 6.

Michuano hiyo inafahamika kama Afcon 2021 licha ya kwamba itafanyika Januari 2022 baada ya mwaka jana kuahirishwa kutokana na janga la virusi vya corona.

Nahodha wa Arsenal ambaye pia ni nahodha wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang ni miongoni mwa mastaa watakaomweka kocha Mikel Arteta kwenye wakati mgumu katika kipindi hicho cha mwaka mpya, huku wakali wengine watakaokosekana huko Emirates kwa kipindi cha michuano hiyo ni Muivory Coast, Nicolas Pepe, Mghana Thomas Partey na staa wa Misri, Mohamed Elneny.

Hata hivyo, Arsenal si wenyewe tu kwenye Ligi Kuu England watakaoathirika kwa kiasi kikubwa na michuano hiyo itakayoanza Januari baada ya Watford kuwa na wachezaji watano ambao wanaweza kuitwa na timu zao za taifa.

William Troost-Ekong, Ismaila Sarr, Imran Louza, Adam Masina, Emmanuel Dennis wote hao wanaweza kuitwa na timu zao za Afrika na kumwaacha kocha Claudio Ranieri kwenye wakati mgumu katika kujiweka pazuri kwenye Ligi Kuu England.

Crystal Palace itakosa mastaa wanne, Wilfried Zaha, Jeffrey Schlupp, Jordan Ayew, Cheikhou Kouyate ambao pia wanaweza kwenda kupiga mzigo kwenye Afcon 2021, jambo ambalo linaweza kuwa pigo kubwa kwa kocha Patrick Vieira.

Kuna timu kibao zinajiandaa na kupoteza wachezaji wake muhimu kwenye michuano hiyo. Timu hizo ni pamoja na Liverpool, ambayo itawapoteza wakali wake Mohamed Salah na Sadio Mane, huku Leicester City itakosa huduma za wakali, Wilfred Ndidi na Kelechi Iheanacho.

Hata hivyo, kuna timu ambazo hazitaathirika na michuano hiyo ya Afrika, ambazo ni Leeds United, Newcastle United, Norwich City na Tottenham Hotspur ambazo kwenye vikosi vyao hakuna wachezaji watakaolazimika kwenda kujiunga na timu zao za taifa za Kiafrika kwa ajili ya mikikimikiki hiyo ya Afcon 2021.

Fainali za Afcon 2021 zitafanyika Cameroon na timu za taifa zinatarajia kupata wachezaji wake wote itakaowatumia kwenye michuano hiyo kabla ya mwaka huu haujamalizika. Jambo hilo linaweza kuwa na madhara makubwa kwenye klabu za Ligi Kuu England, ambapo kwa Desemba kunakuwa na mechi nyingi kabla ya kufika Januari.