Masuaku aumia Afcon 2025 presha ipo Ulaya
Muktasari:
- Beki huyo anayekitumikia kikosi cha DR Congo kwenye Afcon 2025, Masuaku ameripotiwa kupata maumivu ya enka yaliyomfanya ashindwe kumaliza mechi ya Jumamosi iliyopita, alikomea dakika 73 katika sare ya 1-1 dhidi ya Senegal.
RABAT, MOROCCO: SUNDERLAND kijasho kinawatoka baada ya kusikia beki wao Arthur Masuaku amepata majeraha wakati akitumika kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayoendelea huko Morocco.
Beki huyo anayekitumikia kikosi cha DR Congo kwenye Afcon 2025, Masuaku ameripotiwa kupata maumivu ya enka yaliyomfanya ashindwe kumaliza mechi ya Jumamosi iliyopita, alikomea dakika 73 katika sare ya 1-1 dhidi ya Senegal.
Bado haifahamiki ni madhara makubwa kiasi gani ameyapata Masuaku, lakini akizungumzia kuhusu mchezo wa Jumanne dhidi ya Botswana, kocha wa DR Congo, Sebastien Desabre amesema beki huyo hayupo fiti kucheza kwenye mechi hiyo. Desabre amesema: “Vipimo vilionyesha kuna matatizo kidogo kwenye enka. Tutaangalia anavyoendelea.”
Beki Masuaku hatima ya maisha yake huko Sunderland ipo kwenye mashaka makubwa, huku kukiwa na ripoti kwamba huenda akaachana na timu hiyo kwenye dirisha la usajili wa Januari.
Kuumia kwake kunaiweka Sunderland kwenye wakati mgumu wa kufanya biashara ya mchezaji huyo kwenye dirisha la Januari, lakini kocha Regis Le Bris anaamini hilo linaweza kutokea.
Beki huyo wa Sunderland amesema: “Eneo lenye ushindani zaidi kwenye kikosi chetu ni beki, tuna wachezaji wengi wazuri. Vita ni kali, hivyo kwa Arthur, hata kama ni mchezaji mzuri, hakuwa na nafasi nyingi sana kwenye kikosi hiki. Lakini, bado ni mchezaji muhimu kwetu.”