Mastaa United kuvishwa majaketi maalumu
Muktasari:
- Kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kilifanya mazoezi yake ya wazi kwenye Uwanja wa Soldier Field, unaomilikiwa na timu ya Chicago Bears ya Marekani.
CHICAGO, MAREKANI: MASTAA wa Manchester United watafanya mazoezi wakiwa na jaketi maalumu za kupoza hali ya joto kali kwenye ziara yao ya pre-season huko Marekani.
Kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kilifanya mazoezi yake ya wazi kwenye Uwanja wa Soldier Field, unaomilikiwa na timu ya Chicago Bears ya Marekani.
Na licha ya hali ya joto kuwa kali huko Kaskazini mwa Marekani, ambapo mapema wiki iliyomalizika ilifikia nyuzijoto 42, lakini mastaa wa Man United wameambiwa hawapaswi kuhofia kwa sababu watavalishwa jaketi maalumu za kiteknolojia zenye rangi ya fedha ambazo zitakabiliana na hali hiyo ya joto kali.
Mkuu wa kitengo cha viwango vya fiziki wa Man United, Ed Leng, aliwaeleza wachezaji faida ya jaketi hizo ambazo sasa zinafahamika kama kifaa muhimu kwenye mazoezi ya wanamichezo.
Mwanzoni wachezaji waliona kama ni kichekesho, lakini baadaye walipoelezwa kwamba jaketi hizo zitawasaidia katika kukabiliana na joto korofi. Na kwamba wachezaji hao watavaa jaketi hizo baada ya mechi za mazoezi wakati wakijifua kwa mashindano maalumu ya Premier League Summer Series, ambapo kete yao ya kwanza ilikuwa kukipiga na West Ham United uwanjani MetLife, New Jersey usiku wa kuamkia leo Jumapili.
Jaketi hizo zimetengenezwa na Adidas na zitatumika na Man United kama sehemu ya kupoza miili na joto kali ikiwa ni teknolojia mpya michezoni.
Ugunduzi huo umefanyika kwa ajili ya kuhakikisha viwango vya wachezaji vinabaki kwenye ubora uleule na pengine kuongezeka bila hofu ya kusumbuliwa na hali ya mazingira ya joto kali.
Teknolojia hiyo imekuwa ikitumika kwa madereva wa F1 na waendesha baiskeli wanaopita kwenye maeneo yenye joto kali, ambapo jaketi hizo zimetengenezwa kwa vifaa vinavyofanya miili kuwa kwenye hali ya ubaridi wakati wakiendelea kufanya mazoezi.
Joto kali lilikuwa shida kwa wachezaji wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani, ambako kocha wa Chelsea, Enzo Maresca alisema haiwezekani kwa wachezaji kufanya mazoezi vizuri kwenye hali ya joto kali.
Adidas, ambao ni washiriki wa muda mrefu wa Fifa, wanatarajia kugawa jaketi hizo wakati wa fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani.