Mastaa sita Ballon d'Or

Friday July 16 2021
ballon pic

PARIS, UFARANSA. KIWANGO bora binafsi na mafanikio ya timu vinaonekana kuchochea ushindani wa nyota sita katika kinyang’anyiro cha tuzo za mwanasoka bora wa dunia za Ballon d’Or.

Hafla ya tuzo hizo ambazo hutolewa kwa washindi wa vipengele tofauti vya soka inatarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu baada ya kuahirishwa mwaka jana kutokana na tatizo la ugonjwa wa Covid-19

Mastaa hao sita ambao wanaonekana kupewa kipaumbele kikubwa katika ushindani huo ni Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Ng’oro Kante, Robert Lewandowski, Kevin De Bruyne na Jorginho.

Nahodha wa Argentina na Barcelona, Lionel Messi anaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuitwaa tuzo hiyo kwa mara ya saba.

Licha ya kutotwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya na taji la Ligi Kuu ya Hispania akiwa na Barcelona, Messi ameonekana kuwa moto wa kuotea mbali akiwa na jezi yake ya timu ya taifa kwenye mashindano ya Copa America yaliyomalizika huko Brazil.

Messi ameiongoza Argentina kutwaa ubingwa wa mashindano hayo pia akiibuka mchezaji bora na mfungaji bora wa mashindano hayo, likiwa ni taji lake la kwanza kubwa kutwaa akiwa na kikosi cha Argentina cha wakubwa.

Advertisement

Ikiwa atafanikiwa kuibuka mshindi wa tuzo hiyo, huu utakuwa ni wa neema kwake hasa ukizingatia juzi amesaini mkataba mpya utakaombakisha Barcelona hadi 2026.

Kitendo cha Chelsea kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu uliomalizika, kinamuweka pia kundini kiungo Ng’olo Kante katika kuwania tuzo hiyo.

Kante amekuwa na msimu bora ndani ya Chelsea akiiwezesha kutwaa taji la Mabingwa wa Ulaya ambapo alionyesha kiwango cha kizuri kilichofanya baadhi wampigie chapuo kushinda Ballon d’Or ingawa anaweza kuangushwa na kutofanya vizuri katika Euro akiwa na Ufaransa

Nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo ni mchezaji mwingine anayepigiwa chapuo kutokana na mafanikio yake binafsi aliyopata ingawa anaweza kuangushwa na kutofanya vizuri kwa timu zake kuanzia klabu Juventus hadi taifa Ureno.

Ronaldo amemaliza msimu wa 2020/2021 akiwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Italia na pia ameisaidia Juventus kutwaa Kombe la Coppa Italia huku kwenye Serie A wakiambulia kumaliza katika nafasi ya nne ya msimamo.

Kana kwamba haitoshi, licha ya Ureno kutolewa mapema katika mashindano ya Euro, Ronaldo ameacha alama kwa kuibuka mfungaji bora akipachika mabao matano.

Baada ya kuikosa tuzo ya Ballon d’Or mwaka jana ambapo haikutolewa huku akipewa nafasi kubwa, nyota wa Bayern Munich, Robert Lewandowski ameonekana kuendeleza pale alipoishia kwani ameonyesha makali msimu uliomalizika akiwa na jezi ya klabu na ile ya timu ya taifa.

Nyota huyo wa Poland, ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ujerumani na kiujumla amepachika mabao 48 katika mechi 40 za klabu yake za mashindano mbalimbali.

Ameiongoza Bayern Munich kutwaa taji la tisa mfululizo la Ligi Kuu ya Ujerumani na katika mashindano ya Euro, aliifungia Poland mabao matatu.

Mbali na wanne hao, wachezaji wengine ambao wanaonekana wataleta ushindani katika kuwania tuzo hizo msimu huu ni Kevin De Bruyne wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji pamoja na Jorginho wa Chelsea na timu ya taifa ya Italia, ambaye licha ya kutwaa taji la Euro, kipa Gianluigi Donnarumma ndiye aliyeibuka mchezaji bora Euro.


Advertisement