Mastaa Madrid wakutana kupata mlo pamoja
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Hispania imekuwa haipo katika kiwango chao bora, huku Xabi Alonso akitimuliwa kama kocha mwezi uliopita.
MADRID, ENGLAND: MASTAA wa Real Madrid walikutana kwa ajili ya kupata chakula cha jioni kuweka makubaliano kitu gani cha kufanya kipindi kilichosalia cha msimu huu wa 2025/26.
Miamba hiyo ya Hispania imekuwa haipo katika kiwango chao bora, huku Xabi Alonso akitimuliwa kama kocha mwezi uliopita.
Hata hivyo, bado ina nafasi ya kushinda LaLiga, huku wapinzani wao Barcelona wakiwa wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya miamba hiyo inayofahamika kama Los Blancos.
Lakini, Real Madrid imelazimika kupitia hatua ya mchujo (play-off) ili kusonga mbele 16-Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kikosi kinaamini kuna haja ya kufanya jambo kuhusu mwenendo wao wa kupanda na kushuka.
Kikosi hicho chenye mastaa wengi wakiwemo nyota wa England, Jude Bellingham na Trent Alexander-Arnold, kilikutana kwa ajili ya chakula cha jioni na kupiga picha ya pamoja. Wachezaji hao walizingirwa na mashabiki mitaani walipokuwa wakiingia na kutoka kwenye mgahawa huo.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Kylian Mbappe na Vinicius Jr ndio waliolipia bili ya chakula hicho.
Mashabiki walivutiwa na mkusanyiko huo na wana matumaini kuwa utaongeza mshikamano na kuboresha matokeo uwanjani.
Mmoja alisema: “Inafurahisha kuona umoja wa kifamilia wa Real Madrid.”
Mwingine akaongeza: “Ni jambo la kupendeza kuwaona wakiwa pamoja.”
Wa tatu aliandika: “Hivi ndivyo timu halisi inavyoonekana.”
Na mwingine alitoa maoni: “Hii ni zaidi ya klabu, ni familia.”