Mashine ya mabao yatua Liverpool
Muktasari:
- Fowadi huyo wa Ufaransa chini ya umri wa miaka 21 amesaini mkataba wa miaka sita wa kukipiga huko Anfield hadi 2031.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imemnasa staa wao wa Pauni 79 milioni, straika Hugo Ekitike ikinyakua saini yake kutoka kwenye klabu ya Eintracht Frankfurt.
Fowadi huyo wa Ufaransa chini ya umri wa miaka 21 amesaini mkataba wa miaka sita wa kukipiga huko Anfield hadi 2031.
Liverpool imeipiku Newcastle kwenye vita ya kunasa mshambuliaji na hivyo kukamilisha uhamisho wake wa kutua Anfield kwa ajili ya mikikimikiki ya msimu ujao wa Ligi Kuu England.
Ilianza kumfukuzia tangu kwenye dirisha la Januari na kukamilisha dili baada ya mazungumzo na kocha Arne Slot msimu ulipomalizika.
Ekitike alifunga mabao 22 msimu uliopita kwenye mashindano yote, lakini anaamini inaweza kumsaidia kufikia namba kubwa zaidi kwenye tarakimu zake za ndani ya uwanja.
Liverpool itatanguliza kulipa Pauni 69 milioni kisha itaongoza ziada ya Pauni 10 milioni kama bonasi itakayotokana na kiwango bora cha staa huyo uwanjani.
Kabla ya Ekitike, Liverpool ilikuwa ikimfukuzia staa wa Newcastle United, Alexander Isak, lakini miamba hiyo ya St James' Park iliwajibu kwamba straika huyo hauzwi. Lakini, takwimu zinaonyesha ni Erling Haaland na Kylian Mbappe pekee ndio waliokuwa na rekodi tamu ndani ya uwanja kwa wachezaji wa umri wa miaka 23 kwa miaka ya karibuni.
Manchester United ilifanya jaribio la kumnasa Ekitike katika dakika za mwisho na kuzungumza na mkurugenzi wa michezo wa Eintracht Frankfurt, Markus Krosche, lakini straika huyo akili na malengo yake yalikuwa kwenda Liverpool.
Ekitike sasa atasafiri kwenda Asia kukutana na wachezaji wenzake huko Hong Kong, huku Liverpool ikifanya matumizi kwenye usajili wa dirisha hili la majira ya kiangazi kukaribia Pauni 300 milioni.