Mashabiki Young Boys wakinukisha Villa Park, Malen ajeruhiwa
Muktasari:
- Malen, mwenye umri wa miaka 26, alipata kadhia hiyo akiwa anashangilia mbele ya mashabiki wa Young Boys, baada ya kuifungia Aston Villa bao la kuongoza dakika ya 27. Picha ya video zimeonyesha mshambuliaji huyo alipigwa na kikombe cha plastiki.
Mshambuliaji wa Aston Villa, Donyell Malen, amepata jeraha kichwani baada ya kugongwa na kikombe katika mechi ya Europa League dhidi ya Young Boys ya Uswisi, iliyopigwa jana Alhamisi, Novemba 27, 2025 kwenye Uwanja wa Villa Park.
Malen, mwenye umri wa miaka 26, alipata kadhia hiyo akiwa anashangilia mbele ya mashabiki wa Young Boys, baada ya kuifungia Aston Villa bao la kuongoza dakika ya 27. Picha ya video zimeonyesha mshambuliaji huyo alipigwa na kikombe cha plastiki.
Wachezaji wengine wa Aston Villa pia walionekana kugongwa na vitu vilivyorushwa wakiwa kwenye hatua za kushangilia bao hilo, hali ambayo ilizidi kuwa mbaya kabla ya mapumziko kufuatia Malen kufunga bao la pili.
Akiwa katika harakati za kushangilia bao hilo, Malen alikimbia kuelekea sehemu ile ile ya mashabiki, lakini alisimama ili kuepuka mashabiki wa Young Boys. Hata hivyo, mashabiki hao waliendelea kurusha vitu vingi uwanjani.
Nahodha wa Young Boys, Loris Benito, alijaribu kuwatuliza mashabiki hao, lakini ilishindikana. Baada ya hapo, baadhi ya mashabiki walianza kuvuta viti katika sehemu ya wageni na kuvirusha kwa polisi. Wengine waliokuwa mstari wa mbele walianza kupiga polisi na walinzi wa usalama. Pia, mtu mmoja alionekana kuvutwa kando ya uwanja.
Kutokana na vurugu hizo, mwamuzi alikataa kuendelea na mechi hadi hali itakaporekebishwa. Kwa sababu hiyo, mechi ilisitishwa kwa takriban dakika tano.
Pamoja na yote hayo, bado Aston Villa iliibuka na ushindi wa 2-1, huku Joel Monteiro akifunga bao la kufutia machozi upande wa Young Boys.