Mashabiki wampa ujumbe mzito Arteta
Muktasari:
- Kiungo huyo, Merino, 29, alipangwa sambamba na mchezaji mwenzake wa Arenal, Martin Zubimendi kwenye mchezo wa kimataifa, wakati Hispania ilipoichapa Uturuki 6-0, Jumapili katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Arsenal wanamtaka kocha wao Mikel Arteta kufanya mabadiliko ya kiufundi kwenye kikosi chake baada ya kiungo Mikel Merino kufunga hat-trick huko Hispania.
Kiungo huyo, Merino, 29, alipangwa sambamba na mchezaji mwenzake wa Arenal, Martin Zubimendi kwenye mchezo wa kimataifa, wakati Hispania ilipoichapa Uturuki 6-0, Jumapili katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
Staa wa Barcelona, Pedri ndiye aliyanza kufunga kwenye mechi hiyo, alipotupia nyavuni dakika ya sita tu kabla ya Merino kufunga bao la kwanza baada ya kandanda na pasi nyingi la Wahispaniola hao.
Merino alifunga tena kufanya ubao usomeke 3-0 kwa staili ile, huku safari hii akifunga bao kwa mguu wa kulia.
Staa mwingine wa Barcelona, Ferran Torres alifunga kabla ya Merino kuhitimisha hat-trick yake kwa bao matata kabisa alipofunga kwa shuti la mita 20 na kufanya Hispania kuwa mbele kwa mabao 5-0.
Pedri kisha akafunga bao lake la pili kuhitimisha ushindi huo mnono kwa Hispania. Katika mechi hiyo, Merino alipewa uhuru wa kutawala sehemu ya ushambuliaji kitu ambacho kimewafanya mashabiki wa Arsenal kumtaka kocha wao, Arteta kuiga staili hiyo haraka.
Arsenal amekuwa akitumia fomesheni ya 4-3-3. Lakini, Merino ameonyesha kwamba yeye ni mfungaji hodari, hivyo wamemtaka kocha wao kubadili fomesheni na sasa wametumie 4-4-2, ili kumpa nafasi kiungo huyo kucheza kwenye eneo la ushambuliaji sambamba na Viktor Gyokeres.
Shabiki wa kwanza alisema: “4-4-2 itafiti zaidi Merino na Gyokeres wakicheza kama pacha.”
Shabiki mwingine alisema: “Watu wanaweza kuniona kama vile mimi ni chizi, lakini hebu tumchezesha Merino pale mbele na Gyokeres kwenye 4-4-2.”
Kuna mwingine alisema: “Mshambuliaji wa pili Havertz/Merino acheze nyuma ya Gyokeres itakuwa bora.”
Huku kuna shabiki alisema: “Pengine huu umefika wakati wa Arteta kuanza kutumia 4-4-2 ili amchezesha Merino na Gyokeres pale mbele.”