Mashabiki Sporting wamgeukia Gyokeres
Muktasari:
- Gyokeres amekuwa akijitahidi kulazimisha uhamisho kwenda Arsenal katika dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini vigogo wa Sporting wameendelea kushikilia msimamo wao wa kuhitaji kiasi kikubwa zaidi cha pesa.
LISBON, URENO: MASHABIKI wa Sporting Lisbon wamepaza sauti zao kuhusiana na mshambuliaji wa timu hiyo, Viktor Gyokeres, ambaye anahusishwa kutaka kuondoka katika dirisha hili.
Gyokeres amekuwa akijitahidi kulazimisha uhamisho kwenda Arsenal katika dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini vigogo wa Sporting wameendelea kushikilia msimamo wao wa kuhitaji kiasi kikubwa zaidi cha pesa.
Licha ya Mazungumzo yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya pande mbili bado Gyokeres ameshindwa kurudi mazoezini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao, Ijumaa iliyopita.
Rais wa Sporting, Frederico Varandas, ameweka wazi kwamba Gyokeres atachukuliwa hatua za kinidhamu, kama ataendelea kugoma kurudi mazoezini.
Hata hivyo, siku mbili zilizopita iliripotiwa kwamba Arsenal na Sporting zilikubaliana kuhusu dili hilo ambapo washika mitutu hao watatoa Pauni 55 milioni, pamoja na ziada ya Pauni 7.4 milioni kama ada ya uhamisho ya Gyokeres ambaye atasaini mkataba wa miaka mitano.
Mashabiki wa klabu hiyo kubwa ya Ureno walitoa ujumbe wao juu ya sakata kwa mara ya kwanza katika mechi ya kirafiki dhidi ya Celtic.
Mabango mawili yalionyeshwa katika mechi hiyo kuhusiana na mzozo unaomhusu Gyokeres.
Bango la kwanza kama, lilisema ‘Sijali kwa wale wanaoondoka, nina furaha kwa wale wanaobaki.’
Mashabiki wa Sporting waliweka bango jingine lililomlenga Gyokeres wakati wa kipindi cha pili, ambalo linasomeka ‘Hakuna mtu aliye juu ya maslahi ya klabu, haijalishi ni nani.’
Mabango hayo yanaonyesha kuwa mashabiki wa Sporting wako tayari kuendelea mbele bila Gyokeres, huku matumaini yao ya kumbakisha mshambuliaji huyo nyota yakizidi kupungua.
Gyokeres amekuwa na kipindi cha kuvutia cha miaka miwili katika timu hiyo ya Ureno, akiwa amefunga mabao 97 katika mechi 102.
Alifunga mabao 54 msimu uliopita katika mashindano yote, na anahesabiwa kuwa mmoja wa washambuliaji wenye uwezo mkubwa Ulaya.
Iwapo atakamilisha uhamisho wa kwenda Arsenal, Gyokeres ataondoka Sporting akiwa amechukua mataji mawili ya Ligi Kuu Ureno pamoja na Kombe la FA la nchini humo.
Gyokeres aliwasili Sporting akitokea Coventry kwa dau la Pauni 20 milioni mwaka 2023, baada ya kufunga mabao 43 katika misimu miwili na nusu.
Arsenal pia iko karibu kumaliza uhamisho wa beki wa kati wa Valencia, Cristhian Mosquera, na winga wa Chelsea, Noni Madueke, ambaye anatarajiwa kuhamia London kwa dau la Pauni 52 milioni.