Mashabiki Liverpool washangilia kisa Trent
Muktasari:
- Beki huyo raia wa England alijiunga na Madrid Juni mwaka huu baada ya kudumu kwa miaka 20 akichezea Liverpool, timu ambayo ilimkuza tangu akiwa kijana mdogo.
MADRID, HISPANIA: MASHABIKI wa Liverpool walionyesha kufurahia sana baada ya beki wa zamani ambaye kwa sasa anaicheza Real Madrid, Trent Alexander-Arnold kutoonyesha kiwango bora katika mchezo wake wa kwanza wa La Liga akiwa na timu hiyo.
Beki huyo raia wa England alijiunga na Madrid Juni mwaka huu baada ya kudumu kwa miaka 20 akichezea Liverpool, timu ambayo ilimkuza tangu akiwa kijana mdogo.
Kuondoka kwake kuliibua hisia mchanganyiko, mashabiki wengine walimshukuru kwa huduma yake ya muda mrefu na kuheshimu uamuzi wake wa kuondoka, lakini wengine walibaki na chuki.
Hasira hizo zilijidhihirisha Jumatatu usiku, baada ya Trent kucheza vibaya katika ushindi wa 1-0 wa Madrid dhidi ya Osasuna.
Aliondolewa uwanjani dakika ya 68 baada ya kushindwa kushinda mipira ya kugombania hata mmoja, kupoteza mpira mara 15, na hata kupitwa kirahisi.
Takwimu hizo zilionyesha kuwakosha sana mashabiki wa Liverpool ambao kupitia mitandao ya kijamii walitoa maoni yao.
“Sasa ni raha tu, hatuna tena presha kusema Trent ndiye beki bora wa kulia duniani. Atakuwa Aston Villa ndani ya miezi 18 ijayo,” aliandika shabiki mmoja.
“Hii ni faraja kubwa kutomwona tena akicheza kwetu,” mwingine akaongeza.
“Trent leo ameisaidia Osasuna,” shabiki mmoja alitania.
“Kila siku Trent atakapo haribu, nitakuwa mstari wa mbele kushuhudia,” aliapa shabiki mwingine.
Lakini pia kulikuwa na mashabiki waliobaki na heshima au uvumilivu kwa mchezaji huyo mwenye miaka 26:
“Krosi zake zingine zilikuwa nzuri, ila hakuna aliyekuwa sehemu sahihi kuzipokea.”
“Kuchukua muda kuzoea timu mpya ni jambo la kawaida. Alikuwa mchezaji wa daraja la juu kwetu, na atakuwa mchezaji muhimu kwa Madrid vilevile. Heshimuni mchezaji bora zaidi kutoka akademi yenu.”
Mashabiki wengine walimtetea kwa kusema licha ya krosi zake saba, moja pekee ndiyo iliyofika kwa mchezaji, tatizo kubwa lilikuwa Kylian Mbappe kwani si mshambuliaji mwenye uwezo sana wa kupokea mipira hiyo.
Pia, Trent bado anajifunza mfumo mpya wa Kocha Xabi Alonso na kuelewa mbinu na mikimbio ya wachezaji wenzake.