Martin Zubimendi dili lake hadi Julai

Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Hispania alikuwapo London, Ijumaa iliyopita kwenda kukutana na mabosi wa Arsenal wakati kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kilichokuwa na uhakika mkubwa wa kunasa huduma muhimu kwenye dirisha hili.
LONDON, ENGLAND: DILI la kiungo Martin Zubimendi kutua Arsenal litasubiri hadi Januari licha ya kwamba staa huyo wa Kihispaniola na wakala wake alisafiri hadi London kwenda kumalizia baadhi ya mambo ili atue Emirates akitokea Real Sociedad.
Staa huyo wa kimataifa wa Hispania alikuwapo London, Ijumaa iliyopita kwenda kukutana na mabosi wa Arsenal wakati kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kilichokuwa na uhakika mkubwa wa kunasa huduma muhimu kwenye dirisha hili.
Hata hivyo, Sociedad wanataka dili hilo likamilishwe mwezi ujao ili kuweka sawa rekodi zao za kifedha na mwaka wa fedha wa sasa kwenye soka utafika tamati Juni 30. Arsenal ilitarajiwa kulipa Pauni 51 milioni kama ilivyoelezwa kwenye kipengele kilichopo kwenye mkataba wa kiungo huyo, huku ada ya Zubimendi hadi kutua Arsenal, dili lake litafikia Pauni 55 milioni.
Na kwamba ziada ya Pauni 4 milioni, ingelipwa kwenye malipo ya ziada. Taarifa nyingine zilifichua, Real Madrid ilipanga kuvamia mawindo hayo ya Arsenal baada ya kocha Xabi Alonso kutua Bernabeu, lakini Zubimendi tayari alishafanya uamuzi wa kwenda kukipiga Arsenal muda mrefu uliopita.
Na kuhusu hatima ya kiungo Thomas Partey, mazungumzo ya mkataba wake bado hayajafikia kwenye hatua muhimu na kinachoonekana kwenda kutokea ni kwamba mkali huyo wa kimataifa wa Ghana anaweza kuondoka bure mwishoni mwa mwezi.
Partey, 32, amekuwa na ofa kibao mezani kwake kwa klabu nyingi za Ulaya zikihitaji saini yake ikiwamo Galatasaray na Fenerbahce, lakini hadi sasa bado hajafanya uamuzi wa mwisho aondoke au abaki Arsenal.
Kama Partey ataondoka, Arsenal italazimika kutafuta kiungo wa kuja kuziba pengo lake kwa sababu tayari Jorginho ameshaondoka kwenda Flamengo, licha ya kwamba Zubimendi anaweza kuja kuvaa buti za klabu huyo wa Ghana.
Arsenal inapambana kunasa wachezaji inaowataka kwenye dirisha hili, ambapo Arteta na bosi wa usajili, mkurugenzi wa michezo, Andrea Berta wapo bize kutaka wachezaji muhimu, ikiwamo mastraika na kwenye meza yao kuna wakali RB Leipzig, Benjamin Sesko na Sporting CP, Viktor Gyokeres. Mastraika hao wote, Sesko na Gyokeres wapo tayari kutua Emirates.