Maresca: Hincapie? Ile ni kadi nyekundu
Muktasari:
- Kocha huyo wa The Blues, Maresca alikubaliana na kadi nyekundu ya kiungo Moises Caicedo alistahili kutokana na rafu mbaa aliyomchezea staa wa Arsenal, Mikel Merino.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amelalamika kwenye mechi ya dhidi ya Arsenal, timu zote mbili zilipaswa kumaliza zikiwa na wachezaji 10 uwanjani.
Kocha huyo wa The Blues, Maresca alikubaliana na kadi nyekundu ya kiungo Moises Caicedo alistahili kutokana na rafu mbaa aliyomchezea staa wa Arsenal, Mikel Merino.
Lakini, kocha Maresca alisema kwa msisitizo beki wa Arsenal, Piero Hincapie naye alipaswa kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na kiwiko alichompiga Trevoh Chalobah kilichomwacha beki huyo wa The Blues na majeraha jichoni, lakini aliishia tu kuonyeshwa kadi ya njano.
Nahodha wa Chelsea, Reece James alisema kulipaswa kuwa na kadi nyingine nyekundu na Maresca alisisitiza hilo aliposema:
“Nakubaliana na Reece. Sisi makocha, tunashindwa kuelewa kwanini hukumu zinakuwa tofauti. Chalobah aliumia jichoni. Lakini, hukumu ilikuwa tofauti.
“Moises ilikuwa kadi nyekundu. Lakini, ilikuwa hivyo pia kwa Rodrigo Bentancur tulipocheza dhidi ya Spurs. Napata shida sana kuelewa. Nadhani tulipokuwa 11 kwa 11, tulikuwa na timu bora dhidi yao. Tulitawala mchezo, tulimiliki mchezo na kutengeneza nafasi. Kadi nyekundu ilibadili mwenendo wa mchezo kiasi, lakini wachezaji waliweza kushindana na kuonyesha ubora.”
Kiungo wa Arsenal, Merino, ambaye alifunga bao la kusawazisha, alisema:
“Nilihisi enka yangu imetoka, lakini bahati nzuri nina enka na mwili unaonyumbulika. Nilitambua ni rafu mbaya na ilikwenda kuwa kadi nyekundu.”
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alikiri kikosi chake kukosea kwa kuangusha poinri mbili katika mechi hiyo licha ya kwamba bado inaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City inayoshika nafasi ya pili.