Shida ni hii, langoni Chelsea kuna shati
Muktasari:
- Jamie ambaye aliwahi kucheza dhidi ya Chelsea iliyokuwa ya moto hapo zamani, alitoa kauli hiyo baada ya Sanchez kuonyeshwa kadi nyekundu iliyochangia timu yake kupoteza mechi dhidi ya Manchester United.
LONDON, ENGLAND: WIKI kadhaa zilizopita, mchezaji wa zamani wa Liverpool na mchambuzi wa Sky Sports, Jamie Carragher, aliwakasirisha mashabiki wa Chelsea baada ya kusema kipa wao Robert Sanchez na mabeki wao wa kati hawatoshi kuiwezesha timu hiyo kushinda taji lao la kwanza la Ligi Kuu England tangu 2017.
Jamie ambaye aliwahi kucheza dhidi ya Chelsea iliyokuwa ya moto hapo zamani, alitoa kauli hiyo baada ya Sanchez kuonyeshwa kadi nyekundu iliyochangia timu yake kupoteza mechi dhidi ya Manchester United.
Licha ya mashabiki kumpinga, lakini takwimu zinaonyesha kwamba Carragher alikuwa na hoja madhubuti.
Sanchez hayuko kwenye kiwango cha makipa wengine wa timu kubwa zilizomaliza juu ya Chelsea msimu uliopita kuanzia kwa Alisson Becker wa Liverpool, David Raya wa Arsenal na Ederson wa Manchester City.
Kwa takwimu pia inaonyesha mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania hayuko karibu kufikia hata uwezo wa Petr Cech na Thibaut Courtois, waliowahi kuwa makipa namba moja wa timu hiyo.
Takwimu zinaonyesha pia kwamba Sanchez anafikika kirahisi zaidi kutokana na makosa ya mabeki wa kati kuliko makipa wengine wa Chelsea waliotangulia.
Tangu Agosti 2024, Sanchez amefanya makosa matano yaliyopelekea kuzalisha mabao, idadi hiyo ni kubwa zaidi kuliko alivyofanya Raya, Alisson na Ederson wote kwa pamoja.
Vilevile katika kipindi hicho tajwa hapo juu, Raya na Sanchez wamefanya makosa yaliyopelekea mashuti 10 katika magoli yao na matano kati ya hayo yamegeuzwa kuwa mabao na wapinzani wa Chelsea wakati Arsenal ikiwa haijaruhusu hata bao moja kwa makosa hayo.
Sanchez pia ana wastani mdogo sana wa kupiga pasi zilizofika kuliko Alisson na Raya.
Upungufu wa Sanchez katika eneo hilo ilikuwa sababu kubwa kwa Chelsea kujaribu kumsajili kipa wa AC Milan, Mike Maignan, mwanzoni mwa mwaka huu lakini ikafeli.
Ukilinganisha takwimu za usahihi wa pasi kuanzia kwa Cech aliyekuwa langoni wakati Chelsea inashinda taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50 msimu wa 2004/5 ni mkubwa kuliko wa Sanchez.
Vilevile usahihi wa pasi wa Thibaut Courtois tu msimu wa 2016/17 unazidi ule wa Sanchez katika msimu uliopita.
Katika suala la kuruhusu mabao machache pia inaonekana kuwa changamoto kubwa kwa Sanchez na ana wastani mbovu ukilinganisha Cech.
Katika msimu 2004/05, Cech aliruhusu mabao 15 tu rekodi ambayo hadi leo bado haijawahi kuvunjwa.
Hata hivyo, kipa huyu inawezekana akatetewa katika suala hili la kuruhusu mabao kwani ukuta wake hauna mabeki bora kama ilivyokuwa kwa makipa hao awali ambao safu zao za ulinzi zilikuwa zinaundwa na John Terry, Ricardo Carvalho, William Gallas na Gary Cahill, pamoja na mabeki wengine kama Ashley Cole na Cesar Azpilicueta.
Mara kadhaa msimu uliopita kocha Enzo Maresca alikiri kwamba haridhishwi na kiwango ambacho Sanchez anakioyesha.