Maresca awajibu mashabiki Chelsea, atetea umuamuzi wake
Muktasari:
- Chelsea imepoteza mechi hiyo usiku wa jana Jumatano Desemba 3, 2025 ikicheza ugenini Elland Road, na kujikuta ikiporomoka kwa nafasi moja kwenye msimamo wa ligi hiyo kutoka ya tatu hadi nne, kufuatia Aston Villa kushinda mechi yake.
BAADA ya kupoteza mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Leeds United kwa kufungwa mabao 3-1, kocha mkuu wa Chelsea, Enzo Maresca, amewajibu baadhi ya mashabiki wanaolalamikia uamuzi wa kocha huyo wa kutowatumia baadhi ya wachezaji wake muhimu.
Chelsea imepoteza mechi hiyo usiku wa jana Jumatano Desemba 3, 2025 ikicheza ugenini Elland Road, na kujikuta ikiporomoka kwa nafasi moja kwenye msimamo wa ligi hiyo kutoka ya tatu hadi nne, kufuatia Aston Villa kushinda mechi yake.
Maresca amesema wachezaji kama Wes Fofana, Moisés Caicedo na Reece James ni muhimu kwenye kikosi chake, lakini hawezi kuwatumia katika kila mechi, kama mashabiki wa klabu hiyo wanavyopendekeza.
Kocha huyo raia wa Italia amesema ana wachezaji wengi kwenye kikosi chake, hivyo hana ulazima wa kuwatumia kadri anavyotaka kutokana na nafasi na mechi zinazomkabili katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka.
“Tunabadilisha wachezaji kwa sababu tumekuwa tukisema mara nyingi kwamba, kila mchezaji yupo hapa kwa ajili ya Chelsea, na ana uwezo wa kucheza, hivyo ninawatumia kulingana na mechi na uwezo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka.
“Kocha anapobadilisha wachezaji, kunatokana na mambo mengi sana, kuna kiwango kushuka, hitaji la mchezaji kulingana na ugumu wa mechi, kutoa nafasi kwa wachezaji wengine kupumzika kwa ajili ya mechi zinazokuja, kwa hiyo kuna sababu nyingi zinazomfanya kocha kuchukua uamuzi wa kubadilisha kikosi kila mara.
“Wes Fofana, Moisés Caicedo na Reece James ni wachezaji wazuri, lakini aina hii ya wachezaji hatuwezi kuwatumia katika kila mechi. Haiwezekani, kwa sababu vinginevyo wanaweza kuumia tena na kukaa nje kwa miezi mingi,” amesema Maresca.
Ushindi wa 3–1 dhidi ya Chelsea umeifanya Leeds United kujinasua kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja na kuipeleka timu hiyo hadi nafasi ya 17, hatua inayoipa matumaini mapya katika mapambano ya kubaki kwenye Ligi Kuu ya England msimu ujao. Ushindi huo umeongeza morali ndani ya kikosi hicho na kuifanya safari yao kuelekea salama zaidi kwenye nusu ya pili ya msimu.
Kwa upande wa Chelsea, kichapo hicho huenda kikaipa athari timu hiyo ya London, katika mbio za kuendelea kusalia karibu na kilele cha msimamo Ligi, kwani imepoteza pointi muhimu ambazo zingeweza kuiweka karibu na Arsenal ambayo kwa sasa inaongoza msimamo.
Pia huenda ikawa presha kwa kocha Enzo Maresca hasa kutokana na mabadiliko ya kikosi na ukosefu wa uimara katika mechi muhimu. Huku athari nyingine ikitajwa ni kushuka kwa morali ya wachezaji, kwani Chelsea imeonekana kupoteza muunganiko na uthabiti inapokutana na timu zinazopambana vikali.
Kwa ujumla, matokeo hayo yameifanya Chelsea kuhitaji kurekebisha haraka upungufu ilionao kuepuka kupoteza mechi zinazofuata za EPL.