Ndo hivyo: Ghafla tu mipira iliyokufa imegeuka dili Ligi Kuu England
Muktasari:
- Lakini, kwa sasa upepo umegeuka na mipira ya kutenga (set-pieces), kurusha na mipira mirefu ndiyo staili inayotamba kwa sasa.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya miaka kadhaa ya kushuhudia timu za soka zilizokuwa zikitawala dunia ni zile zilizokuwa zikicheza staili ya kupiga pasi nyingi za gonga fupifupi (tiki-taka) kama ilivyokuwa kikosi cha Barcelona chini ya Pep Guardiola.
Lakini, kwa sasa upepo umegeuka na mipira ya kutenga (set-pieces), kurusha na mipira mirefu ndiyo staili inayotamba kwa sasa.
Msimu huu wa 2025/2026 kwenye Ligi Kuu England, timu zimekuwa zikifunga kwa mipira ya kutenga katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa huko nyuma, huku miamba inayoshindania ubingwa, Arsenal ikiwamo na uhodari mkubwa katika mtindo huo wa soka.
Staa wa zamani wa Liverpool, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa Sky Sports, Jamie Carragher alibainisha mshangao wake kuona Arsenal ni timu inayoongoza kwa kufunga mabao kwa set-pieces, aliposema:
“Mimi ni shabiki wa Liverpool, naitazama Arsenal na kila wakati inapopata kona, nashika kichwa. Sijawahi kuona kitu kama hiki kwenye soka. Nadhani hata huko kwa wengine kwenye ulimwengu wa wapenda soka, wanapowaona hawa watu wamepata kona, wanafahamu wazi wanakwenda kufunga.”
Hata hivyo, si kikosi hicho cha Kocha Mikel Arteta pekee kilichoonekana ni tishio kwenye mipira hiyo ya kutenga kwa msimu huu. Iwe kwa mipira ya kona au friikiki, au kwa timu zinazotumia mtindo wa zamani wa Stoke City wa kufunga mabao kwa mipira iliyokuwa ikirushwa na mkali wao Rory Delap, kwa sasa kwenye Ligi Kuu England, kumekuwa na matumizi mazuri ya mipira iliyokufa, timu zimekuwa zikinufaika kuliko huko nyuma.
Lakini, ni mabao kiasi gani yamefungwa kutokana na staili hiyo? Ni timu gani inaoongoza kwa kufunga mabao kutokana na mipira iliyokufa?
Hizi hapa timu zilizoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu wa 2025/2026 kutokana na mipira ya set-pieces, ikiwamo kona, friikiki na penalti.
1. Arsenal - mabao 12
Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Arsenal imefunga mabao 25, huku karibu nusu ya mabao hayo yalifungwa kutokana na mipira iliyokufa na mabao 10 yalifungwa ama kwa kona, friikiki au kurusha na mabao mawili yalifungwa kwa penalti.
2.Chelsea - mabao 10
Katika mechi 13 ilizocheza Chelsea kwenye Ligi Kuu England msimu huu, imefunga mabao 24, huku mabao 10 yalipatikana kwa mipira ya kutenga. Katika mabao hayo ya mipira iliyokufa, penalti ni moja tu, huku mabao tisa yalitokana na ama kona, mipira ya kurusha au friikiki.
3.Crystal Palace - mabao 9
Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi 13 imekusanya pointi 20 na kufunga mabao 17, huku kwenye idadi hiyo ya mabao, tisa yalipatikana kwa mipira iliyokufa na sita yalifungwa ama kwa friikiki, kona au mipira ya kurusha, wakati mabao matatu yalifungwa kwa mikwaju ya penalti.
4.Man United - mabao 9
Manchester United imekusanya pointi 21 katika mechi 13 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ikifunga mabao 21 na kufungwa 20. Katika mabao hayo iliyofunga Man United, tisa yalitokana na mipira iliyokufa, mabao manane yalifungwa ama kwa mipira ya kona, friikiki au mipira ya kurushwa, wakati bao moja tu ndilo walilofungwa kwa penalti.
5.Brentford - mabao 8
Kwenye mechi 13 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England, Brentford imekusanya pointi 19 na imefunga mabao 21 katika ligi, huku mabao manane yalitokana na mipira iliyokufa. Kwenye orodha ya mabao hayo ya mipira iliyokufa, penalti yalifungwa mabao matatu, huku matatu yaliyokana na ama kona, friikiki au mipira ya kurusha.
Sunderland - mabao 8
Sunderland imepanda daraja msimu huu, lakini mambo yake ndani ya uwanja ni moto kwelikweli, ikikusanya pointi 22 katika mechi 13 ilizocheza, pointi nane tu nyuma ya vinara Arsenal. Kwenye mechi hizo, Sunderland imefunga mabao 17, huku manane yakitokana na mipira iliyokufa na penalti ni mbili, huku sita yalitokana na ama mipira ya kurusha, friikiki au kona.