Marekani yatoa onyo kwa wapinzani Kombe la Dunia ikiizamisha Paraguay 4-1
Muktasari:
- Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa SoFI jijini Los Angeles, Marekani imetumia dakika 45 za kwanza kutengeneza mabao yake matatu ya ushindi huo ikitawala mchezo huo vizuri kwa kuwabana Paraguay.
Timu ya Taifa ya Marekani, (The Yanks) imeanza vyema Fainali za Kombe la Dunia 2026 ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Paraguay.
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa SoFI jijini Los Angeles, Marekani imetumia dakika 45 kutengeneza mabao matatu ya ushindi huo ikitawala mchezo vizuri kwa kuwabana Paraguay.
Wenyeji wamepata bao la kwanza dakika ya saba kwa bao la kujifunga kupitia beki wa Paraguay, Damian Bobadilla,wakati akipambana kuzuia shambulizi la Marekani.
Mshambuliaji Folarin Balogun ameweka kambani mabao mawili dakika za 31 na 45+5 kuhitimisha ushindi huo kwa taifa lake likimaliza kipindi cha kwanza.
Balogun ambaye ni mshambuliaji wa Monaco ya Ufaransa amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili kwenye fainali hizo za mwaka 2026 ambapo ilibaki kidogo atengeneze hat trick ya kwanza, lakini bao lake la kwanza dakika ya 28 lilikataliwa kutokana na kuotea.
Paraguay imefanikiwa kupata bao la kufuatia machozi kupitia kiungo Mauricio Prado aliyetokea benchi akitumia asisti ya Julio Enciso.
Wakati mchezo huo ukielekea mwisho kiungo wa Marekani, Giovan Ryna amepigilia msumari wa mwisho kwa bao la kiufundi akifunga kwa shuti la 'kibao'.
Marekani imekuwa timu ya kwanza kupata ushindi mkubwa tangu kuanza kwa fainali hizo ambapo mpaka sasa hakuna mechi iliyozalisha mabao mabao mengi ya ushindi kama huo.