Viatu vya Kane, Bellingham vyaibwa kambini Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na mtandao wa Daily Mail, wizi huo ulitokea wakati mzigo wa timu hiyo ukiwa safarini kutoka West Palm Beach, Florida kuelekea kituo cha mazoezi cha Swope Soccer Village kilichopo Missouri ambako England itakuwa kambini kwa angalau wiki tatu zijazo.
KANSAS CITY, MAREKANI: KIKOSI cha England kimejikuta kwenye taharuki wakati wakijiandaa mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 ambao utachezwa Jumatano, Juni 17 dhidi ya Croatia baada ya vifaa muhimu vya mazoezi na viatu vya baadhi ya nyota wake kuibwa wakati vikisafirishwa kwenda kambi yao ya Kansas City, Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na mtandao wa Daily Mail, wizi huo ulitokea wakati mzigo wa timu hiyo ukiwa safarini kutoka West Palm Beach, Florida kuelekea kituo cha mazoezi cha Swope Soccer Village kilichopo Missouri ambako England itakuwa kambini kwa angalau wiki tatu zijazo.
Miongoni mwa vitu vilivyoibwa ni viatu vya wachezaji maarufu akiwemo nahodha wa timu hiyo, Harry Kane pamoja na kiungo nyota Jude Bellingham.
Pia mipira rasmi ya mashindano, vifaa vya mazoezi, vifaa vya uchambuzi wa video, meza za tiba na hata ubao wa kocha Thomas Tuchel zimeripotiwa kutoweka.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa wakati mzigo ulipowasili Kansas City, wafanyakazi wa timu walikuta mpira mmoja pekee umebaki huku sehemu kubwa ya vifaa muhimu ikiwa haipo.
Tukio hilo limezua hofu ndani ya kambi ya England huku maofisa wa Shirikisho la Soka la England (FA) wakishirikiana na polisi wa eneo hilo kufanya uchunguzi ili kubaini waliohusika.
Polisi wa Kansas City wamethibitisha kuwa tayari wameanza uchunguzi wa tukio hilo na kwamba mtu mmoja ameripotiwa kukamatwa kuhusiana na sakata hilo.
"Tunachunguza uwezekano wa wizi wa vifaa kutoka kwenye gari la timu lililowasili Kansas City huku baadhi ya vitu vikiwa havipo. Uchunguzi bado unaendelea," ilisema sehemu ya taarifa ya polisi.
Ripoti zimeeleza kuwa maofisa wa usalama wanachunguza uwezekano wa baadhi ya madereva waliokuwa wameaminiwa kusafirisha vifaa hivyo kuhusika katika tukio hilo.