Marekani wazindukia kwa Iran Olimpiki

Muktasari:

  • Czech itacheza na Marekani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Iran pointi 84:78, mshindi wa mechi hiyo atakuwa na nafasi kubwa ya kutinga kwenye hatua ya mtoano.

Ushindi wa pointi 120-66 dhidi ya Iran umefufua matumaini ya kusonga mbele kwa timu ya kikapu ya wanaume ya Marekani kwenye moja ya mechi za kundi A leo kwenye  michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini Japan.

Timu hiyo iliyoanza kwa kipigo dhidi ya Ufaransa kwenye michezo hiyo, leo imemalizia hasira zake kwa Iran na kufufua matumaini ya kusonga hatua ya mtoano kwenye kundi lao.

Shujaa wa Marekani katika mchezo huo alikuwa Damian Lillard aliyeongoza kwa kufunga pointi 21 peke yake wakati Devin Booker akifunga pointi 16 na kuchukua rebounds mara tano.

Marekani yenye historia ya kuwa mabingwa kwenye michezo mitatu iliyopita ya Olimpiki itaigia kwenye hatua ya mtoano kama itashinda mechi yao ya mwisho ya dhidi ya Jamhuri ya watu wa Czech Jumamosi katika mechi za kundi A.

Ujerumani pia iko katika hatua nzuri ya kuingia kwenye mtoano baada ya kuichapa Nigeria 99-92 kwenye kundi B.

Johannes Voigtmann ndiye alikuwa mfungaji bora wa Ujerumani akitupia pointi 19 peke yake katika mchezo huo wa pili kwa Ujerumani ambayo ilianza kwa kuichapa Italia katika mchezo wa ufunguzi Jumapili iliyopita.

Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Nigeria ambayo pia imefungwa na Australia pointi 84-67 kwenye kundi B, mchezo ulifanyika kwenye dimba la Saitama Super Arena.