Mapema tu kocha Asec aanza sababu dhidi Simba CAFCL

Muktasari:
- Lakini, bado wamebakiwa na Serge Pokou aliyewafunga Simba mara ya mwisho Kwa Mkapa naye akiwa na rekodi ya kuwa na mabao manne katika ligi, huku kimataifa akiwa nalo moja. Asec wana pointi 10 na tayari wameshafuzu robo fainali.
Kocha wa Asec Mimosas, Juliet Chevalier amesema mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba inampa presha kutokana na hesabu zao, lakini wana pigo la kumkosa mshambuliaji hatari Sankara Karamoko mwenye rekodi ya kufunga mabao manne katika mechi nne za michuano hiyo na saba katika ligi.
Lakini, bado wamebakiwa na Serge Pokou aliyewafunga Simba mara ya mwisho Kwa Mkapa naye akiwa na rekodi ya kuwa na mabao manne katika ligi, huku kimataifa akiwa nalo moja. Asec wana pointi 10 na tayari wameshafuzu robo fainali.

Safu ya ushambuliaji mpya ya Simba yenye pointi tano kwenye nafasi ya pili, inabebwa na Freddy Koublan mwenye bao moja na Pa Omary Jobe akiwa na mawili mpaka sasa katika mechi tano za michuano yote walizocheza kila mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema Simba itataka kushinda na watacheza mechi hiyo kama fainali wakati wao wanataka alama angalau mbili au tatu kwenye mechi mbili zilizosalia ili waongoze kundi hilo.
"Nilikuwa kwenye wiki mbili nzito za kuijenga upya safu yangu ya ushambuliaji bila Sankara Karamoko ambaye ameshauzwa katika usajili wa dirisha dogo kwenye timu ya Wolfsberger AC inayocheza katika Ligi Kuu ya Austria.

"Wakati wapinzani wetu wana watu na timu mpya tofauti na ile tuliyokutana nayo kabla, hivyo haitakuwa mechi rahisi, lakini tutakuwa katika uwanja wa nyumbani," alisema kocha Juliet.
Asec inaongoza kundi B ikiwa na pointi 10 ikifuatiwa na Simba yenye tano na katika mechi nne za mwisho za ligi imeshinda mara mbili zote ikiwa nyumbani, huku ugenini ikiwa imepoteza michezo miwili. Rekodi za Simba zinaonyesha kuwa kila inapokutana nao katika uwanja wao haijawahi kuachwa salama.
Nako kwa Wekundu wa Msimbazi mambo yanajirudia kwani katika mechi mbili za mwisho walizocheza nao kwa Mkapa wamewafunga mabao 3-1 na sare ya bao 1-1.
Kutokana na rekodi hizo za kutotoka salama ugenini, Simba inaonekana kuwa na kazi ya ziada katika mechi hiyo itakayochezwa Ijumaa, Februari 23 nchini Ivory Coast na imetumia muda mwingi kujiandaa huku ikiahirishiwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa.
KUNDI B
P PTS
Asec 4 10
Simba 4 5
Jwaneng 4 4
Wydad 4 3