Manchester United yatoa msimamo ishu ya Bruno
Muktasari:
- Uongozi wa Mashetani Wekundu unataka kuhakikisha Bruno anasalia Old Trafford kwa muda mrefu kutokana na mchango wake katika safu ya kiungo na uongozi wake uwanjani.
MANCHESTER United inapanga kuanza mazungumzo ya mkataba mpya na kiungo wa kimataifa wa Ureno, Bruno Fernandes, 31, mara tu zitakapomalizika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.
Uongozi wa Mashetani Wekundu unataka kuhakikisha Bruno anasalia Old Trafford kwa muda mrefu kutokana na mchango wake katika safu ya kiungo na uongozi wake uwanjani.
Fernandes amekuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa Man United katika misimu ya karibuni, hivyo klabu hiyo inataka kumlinda asiondoke na ipo tayari kumpa hata nyongeza ya mshahara asiende kokote.
Mara kadhaa staa huyo amekuwa akihusishwa na vigogo wa Saudi Arabia ambao mwaka jana walikuwa tayari kutoa zaidi ya Pauni 90 milioni ili kumnunua na kumpa mshahara takribani mara nne ya ule ambao anaupata kwa sasa.
Bruno mwenyewe kipaumbele chake cha kwanza ni kuendelea kusalia Man United, lakini kwa sharti la timu hiyo kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Elliot Anderson
MANCHESTER City inadaiwa kuwa karibu kukamilisha dili la kumsajili kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Elliot Anderson dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa kuwa Anderson, 23, anaipa kipaumbele zaidi Man City badala ya Manchester United ambao pia wamekuwa wakifuatilia maendeleo yake. Hata hivyo, Nottingham Forest imeweka wazi kuwa haipo tayari kumuachia kirahisi nyota huyo.
Piero Hincapie
ARSENAL inadaiwa imefikia hatua nzuri ya usajili wa moja kwa moja wa beki wa kimataifa wa Ecuador, Piero Hincapie, 24, kutoka Bayer Leverkusen.
Taarifa zinaeleza Hincapie anatarajiwa kusaini Arsenal kwa uhamisho wa kudumu mara tu msimu utakapomalizika, kwani benchi la ufundi limevutiwa na kiwango alichoonyesha tangu ajiunge kwa mkopo katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Martin Odegaard
MABOSI wa Arsenal wanafikiria kuuza baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na mmoja kati ya mastaa yao ni kiungo Martin Odegaard pamoja na Gabriel Martinelli.
Inaelezwa Washika Mitutu hao wanataka kuuza kwanza kabla ya kusajili kwa sababu wanahitaji kukusanya pesa kwanza kwani idadi kubwa ya mastaa wanaowahitaji wanauzwa kwa bei mbaya.
Kim Min-jae
CHELSEA imeanza mazungumzo na wawakilishi wa beki wa kati wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Korea Kusini, Kim Min-jae, 29.
Kim Min-jae ana uzoefu mkubwa wa soka la ushindani Ulaya na amewahi kung’ara Serie A kabla ya kujiunga na Bayern.
Chelsea inaamini Kim ana uzoefu ambao utasaidia wachezaji vijana katika safu ya ushambuliaji. Bayern haijaonyesha dalili za kumuachia.
Aleksandar Pavlovic
VIGOGO wa Ligi Kuu England, Chelsea na Manchester City wanatajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa karibu kiungo wa Bayern Munich, Aleksandar Pavlovic, 21.
Taarifa zinaeleza Bayern inaweza kuhitaji takriban Euro 65 milioni ili kumruhusu kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani kuondoka.
Pavlovic ambaye msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote, mkataba wake unaisha 2029.
Yan Diomande
LIVERPOOL inaripotiwa kumuweka kwenye rada winga chipukizi wa RB Leipzig, Yan Diomande, 19, kama mbadala wa muda mrefu wa supastaa Mohamed Salah ambaye anaweza kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Taarifa zinaeleza kuwa Liverpool inamuona Diomande ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuchukua nafasi ya Salah siku zijazo kutokana na kiwango chake alichoonyesha akiwa na RB Leipzig.
Samuel Amissah
VIGOGO wa Ligi Kuu England Arsenal, Manchester United na Chelsea wanatarajiwa kuingia kwenye vita ya usajili kwa ajili ya beki wa kati wa timu ya vijana ya Fulham chini ya miaka 21, Samuel Amissah, 18, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Amissah ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika timu za vijana mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote.