Manchester United yatenga mshahara mnono kwa Varane

Monday July 19 2021
man u pic

MANCHESTER ENGLAND. VITA ya pesa. Unaambiwa endapo dili la beki kisiki wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Raphael Varane kujiunga na Manchester United litakamilika katika dirisha hili, fundi huyo atakunja mshahara mnono mara mbili ya ule anaoupata sasa akiwa na Madrid.

Taarifa kutoka England zimefafanua kwamba Man United inataka kumpa staa huyo ofa ya mshahara wa Pauni 10.2 milioni kwa mwaka.

Mashahara huo unaondoa kabisa matumaini ya Madrid kuendelea kubaki na staa huyo kwa msimu ujao na unazidisha taarifa za kwamba dili hilo linaweza kukamilika ndani ya wiki hii ikiwa Man United itawasilisha ofa ya Pauni 50 milioni inayohitajika na Madrid.

Mshahara wa sasa wa fundi huyo ni Euro 5 milioni kwa mwaka ambapo Madrid baada ya kuona Man United inamnyemelea imepanga kumsainisha mkataba mpya utakaomuwezesha kupata Euro 7 milioni, kiasi ambacho bado ni kidogo.

Varane ameripotiwa kuwa na hasira kutokana na mshahara anaoupata ukilinganisha na mishahara ya wachezaji wapya kama David Alaba ambaye atalipwa Euro 12 milioni kwa mwaka, hivyo anaangalia timu itakayokuwa tayari kumpa mshahara mnono ndio ajiunge nayo katika dirisha hili.

Madrid imekuwa ikijaribu kumshawishi aongeze mkataba na ikiwa itashindwa kufanya hivyo italazimika kumuuza kabla ya dirisha kufungwa kwani mkataba wake unamalizika mwaka 2022, hivyo ataondoka kwa pesa kiduchu katika dirisha dogo la Januari ama bure kabisa katika dirisha la mwisho wa msimu mkataba wake utakapoisha.

Advertisement

Kwa upande wa Manchester United yenyewe imeripotiwa kuwa kwenye mpango wa kuwasilisha ofa nono kwenye wiki hii ili kujihakikishia huduma yake kwa msimu ujao.

Mazungumzo baina ya wawakilishi wa mchezaji huyu na Man United yameripotiwa kwenda sawa lakini jambo linaloonekana kuwa linasumbua ni Man United kuhitaji kupunguziwa bei na Madrid.

Dau la sasa la Pauni 50 milioni linaonekana kuwa kubwa ukizingatia ina mpango pia wa kumsajili Kieran Trippier kutoka Atletico Madrid na wakati huo haijauza mchezaji yoyote.

Licha ya kuwepo kwa mazungumzo baina ya wahusika wa Man United na AC Milan kwa ajili ya kumuuza Alex Telles, Milan inaonekana kuhitaji zaidi kumsajili kwa mkopo. Vilevile Diogo Dalot naye bado hakuna timu yoyote iliyowasilisha ofa mezani ili kumsajili.

Mchezaji mwingine anayeweza kunenepesha mfuko wa timu hiyo na kuifanya imalizane na Madrid mapema ni Axel Tuanzebe anayewindwa vikali na Newcastle lakini nayo inamuhitaji kwa mkopo.

Man United imeendelea kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao ambapo asilimia kubwa ya wachezaji wake wameshaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu.

Miongoni mwa maeneo yaliyoonekana kuwa na upungufu mkubwa katika msimu uliopita ilikuwa ni lile la ulinzi ambalo msimu huu ndio mabosi wa timu hii wanapambana vya kutosha kusajili wachezaji waliopendekezwa na kocha kama sehemu ya maboresho.

Varane ni mmoja ya wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha Madrid ambaye kama ataondoka atakuwa ni mchezaji wa pili tegemeo kuondoka kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya Sergio Ramos aliyejiunga na PSG kwa usajili huru mara baada ya kufikia uamuzi wa kutosaini mkataba mpya mwisho wa msimu.

Advertisement