Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manchester United yatema kibao

MAN UTD Pict

Muktasari:

  • Kipa veterani, Tom Heaton naye pia mkataba wake unaelekea mwisho, lakini klabu imeripotiwa kuwa kwenye mazungumzo ya kutaka kumsainisha dili jipya.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imethibitisha itawatema mastaa wake Christian Eriksen, Jonny Evans na Victor Lindelof kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya mikataba yao kumalizika.

Kipa veterani, Tom Heaton naye pia mkataba wake unaelekea mwisho, lakini klabu imeripotiwa kuwa kwenye mazungumzo ya kutaka kumsainisha dili jipya.

Wachezaji wengine watakaofunguliwa mlango wa kutokea ni wa kwenye akademia ambao ni Hubert Graczyk, Jack Kingdon, Sam Murray, Tom Myles, James Nolan na Tom Wooster.

Beki wa kimataifa wa Sweden, Lindelof alijiunga na Man United akitokea Benfica mwaka 2017 na ameitumikia timu hiyo katika mechi 284 kwa kipindi cha misimu minane. Alikuwamo kwenye kikosi kilichoshinda Kombe la Ligi 2023 na Kombe la FA 2024 na kile kilichopoteza kwenye fainali ya Europa League 2021 na 2025.

Kiungo Eriksen alifunga kwenye mechi yake ya 108 ambayo ilikuwa ya mwisho kwenye klabu ya Man United ilipocheza na Aston Villa katika siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu England 2024-25.

Staa huyo wa zamani wa Ajax, Tottenham na Inter Milan alijiunga na Man United mwaka 2022 baada ya kucheza kwa muda mfupi Brentford na ilikuwa klabu aliyocheza baada ya kurudi kwenye soka kufuatia kupatwa na shambulio la moyo akiwa uwanjani kwenye michuano ua Euro 2021.

Evans atastaafu soka baada ya kurejea Man United kwa mara ya pili mwaka 2023. Beki huyo mwenye umri wa miaka 37 ni zao la akademia ya Man United na ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu England na alibeba Kombe la FA aliporudi kwa mara ya pili klabuni hapo. Alizichezea pia Sunderland, West Brom na Leicester City kwenye maisha yake ya soka.

Kipa Heaton, naye alitokea kwenye akademia ya Man United, alirejea kujiunga na timu hiyo mwaka 2021 baada ya kuondoka 2010. Baada ya mikopo kadhaa alijiunga jumla Cardiff, Bristol City, Burnley na Aston Villa na alicheza mechi tatu tu tangu aliporudi Old Trafford. Kocha Ruben Amorim anataka kumbakiza kipa huyo kutokana na uzoefu wake ili kuwapa ujuzi makipa vijana.

Kwa makinda sita wa akademia ambao watafunguliwa mlango wa kutokea, hakuna aliyepata bahati ya kucheza kikosi cha kwanza cha Man United, hivyo wameachwa wakapate nafasi huko kwingine.