Manchester City yamwekea ulinzi Haaland

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER City imetuma mtu wake wa viungo Mario Pafundi kwenda kwenye kambi ya timu ya taifa ya Norway kwa ajili ya kazi moja tu, kumfuatilia straika wao, Erling Haaland.

Mabingwa hao wa England wanavutiwa na ubora wa straika wao huyo mpya waliyemsajili kwenye dirisha lililopita baada ya kufunga mabao 14 katika mechi tisa alizocheza hadi sasa.

Kutokana na hilo, Man City wanataka kufuatilia utimamu wa Haaland hata anapokuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa.

Miamba hiyo ya Etihad ilimsajili Haaland kwa ada ya Pauni 51.4 milioni kutoka Borussia Dortmund na wanafahamu wazi majeruhi yalitibua mambo yake katika miaka yake ya mwisho huko Ujerumani.

Katika kufanya mambo hayajirudii, wametuma mtaalamu wao wa viungo kwenda kumfanyisha mazoezi mshambuliaji huyo hata kama yupo kwenye majukumu ya timu ya taifa.

Kocha wa Norway, Stale Solbakken alisema Pafundi atafanya kazi kama kocha wao wa viungo wa tatu na majukumu yake yatakuwa kwa timu nzima si Haaland peke yake.

Hata hivyo, kocha huyo amekiri uamuzi huo umefanywa baada ya Haaland kuomba mtaalamu huyo wa viungo kutoka Man City ajumuishwe kwenye benchi la ufundi la timu ya taifa.

Norway inajiandaa na mechi za michuano ya UEFA Nations League dhidi ya Serbia na Slovakia.

Haya ni mapumziko ya kwanza ya mechi za kimataifa kwa Haaland tangu alipojiunga na Man City na makocha wa Etihad wapo tayari kutengeneza uhusiano mzuri na wale wenzao wa timu ya taifa kwa ajili ya maslahi ya mchezaji huyo.

Haaland atakuwa nahodha wa Norway endapo kama kiungo wa Arsenal, Martin Odegaard hatacheza mechi hizo.