Man United yamaliza utata dili la Bruno
Muktasari:
- Fernandes alijiunga na Man United akitokea Sporting CP, Januari 2020 kwa ada ya Pauni 67.7 milioni na tangu wakati huo amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo sana wa Man United.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imechukua hatua kuhakikisha inamaliza sintofahamu kuhusu mustakabali wa nahodha wao wa raia wa Ureno, Bruno Fernandes.
Hapo awali, Man United ilidaiwa ilikuwa tayari kumuuza Fernandes kwenda Al-Nassr FC ya Saudi Arabia kufuatia ofa ya Pauni 80 milioni, lakini alishawishiwa kubaki na aliyekuwa kocha mkuu wa wakati huo Ruben Amorim.
Safari hii, viongozi wa klabu wamemhakikishia Fernandes hawataki kumuachia kwa hali yoyote hasa baada ya nyota huyo kueleza aliumizwa na nia ya klabu kutaka kumuuza mwaka jana.
Viongozi wa Man United wamemwambia wazi wanataka awe kiungo muhimu katika kujenga mafanikio ya timu hiyo.
Bruno, 31 ni miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Professional Footballers' Association (Mchezaji Bora wa Mwaka).
Mkataba wa Fernandes una kipengele cha kuruhusiwa kuondoka ikiwa klabu inayomhitaji italipa Euro 65 milioni, lakini timu inayotaka kumsajili itatakiwa kutoka nje ya England.
Hata hivyo, Bruno mwenyewe ameonyesha kuridhishwa na kubaki Man United, huku uongozi ukiamini kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya kutaimarisha zaidi uamuzi wake wa kubaki.
Kwa sasa Man United inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, ambayo msimu huu timu tano za juu zitafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Fernandes ana mkataba na Man United hadi mwaka ujao, lakini klabu ina chaguo la kumuongezea mwaka mmoja zaidi.
Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chelsea kipa wa Man United Senne Lammens alidokeza kuwa nahodha huyo bado ana nia ya kubaki.
Fernandes alijiunga na Man United akitokea Sporting CP, Januari 2020 kwa ada ya Pauni 67.7 milioni na tangu wakati huo amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo sana wa Man United.