Bruno aibana Man United, aweka masharti magumu
Muktasari:
- Kwa sasa, hatma ya Bruno bado haijawa wazi, lakini kilicho dhahiri ni msimu ujao unaweza kuwa wa maamuzi makubwa kwake na kwa klabu hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, ameweka wazi mustakabali wake ndani ya klabu hiyo utategemea uwezo wa timu hiyo kurejea katika ushindani wa mataji msimu ujao.
Nyota huyo wa Ureno, aliyejiunga na United kutoka Sporting Lisbon Januari 2020, amekuwa mhimili mkubwa wa kikosi hicho, lakini bado ana zaidi ya mwaka mmoja katika mkataba wake, hali inayozua sintofahamu kuhusu hatma yake.
Bruno amekiri msimu uliopita alikataa ofa nono ya Pauni 700,000 kwa wiki kutoka klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia, lakini bado anaendelea kutathmini mustakabali wake huku klabu mbalimbali kubwa Ulaya zikionyesha nia ya kumtaka.
Taarifa zinaeleza Fernandes pia anafikiria kwa uzito uwezekano wa kuondoka, ingawa ofa kubwa kutoka Saudi Arabia bado ipo mezani kwake, pia klabu kubwa Ulaya zinaweza kutumia kipengele chake cha kuvunja mkataka kwa Pauni 57 milioni.
Akiwa na mabao manane na asisti 17 katika Ligi Kuu England msimu huu, Fernandes ameendelea kuwa tegemeo kubwa kwa United katika harakati zao za kumaliza katika nafasi za juu.
“Kila anayekuja Manchester United anataka kushinda kila taji,” amesema katika mahojiano na The Sunday Times wiki iliyopita ambayo yameibua hoja huenda sasa umefika wakati wa kufikiria kuondoka katika timu hiyo ambayo mara ya mwisho ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2012/13 katika utawala wa Sir Alex Ferguson.
“Na kila nilipoongea na klabu, nilisema ninachotaka ni kushindana. Kwa sababu nikishindana, nitakuwa karibu kushinda. Nisipo shindana, hakuna nafasi ya kushinda taji lolote,” amesema.
Hata hivyo, inaripotiwa Man United wanataka kumbakiza nyota huyo, lakini huenda wakalazimika kumpa mkataba mpya wenye mshahara mkubwa zaidi ili kumshawishi kubaki Old Trafford.
Kwa sasa, hatma ya Bruno bado haijawa wazi, lakini kilicho dhahiri ni msimu ujao unaweza kuwa wa maamuzi makubwa kwake na kwa klabu hiyo.