Chelsea kumweka sokoni Garnacho, sababu yatajwa
Muktasari:
- Garnacho na wenzake walikuwa mzigoni jana dhidi ya Brighton ambao walitoka sare ya mabao 2-2 na Tottenham Hotspur wikiendi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA wapo tayari kumuuza winga Alejandro Garnacho msimu huu wa majira ya joto, kwa mujibu wa talkSPORT, ambapo uongozi wa klabu umetambua kuwa usajili wake wa Pauni 40 milioni haujaenda kama ilivyotarajiwa.
Hilo ni anguko kubwa kwa Garnacho ambaye alijiunga na klabu hiyo Agosti, mwaka jana, kutoka Manchester United, ambako alionyesha kiwango bora, lakini hakufaa katika mfumo wa kocha Ruben Amorim ambaye naye ameshafurushwa Old Trafford.
Tangu ahamie Stamford Bridge mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 ameshindwa kufikia matarajio ya mabosi wa klabu, kwani amefunga mabao manane na asisti nne katika mashindano yote, lakini akiwa na michango mitano tu ya mabao aliyootoa katika Ligi Kuu England.
Zaidi ya hapo, mabao manne aliyofunga yalikuwa katika michezo ya vikombe vidogo kama Carabao na FA dhidi ya timu za madaraja ya chini zikiwamo Wrexham AFC, Port Vale na Cardiff City.
Uamuzi huo wa Chelsea unakuja baada ya Garnacho kucheza vibaya dhidi ya klabu yake ya zamani katika kipigo cha bao 1-0 wikiendi iliyopita, . alipoingia katika dakika ya 16 baada ya kiungo Estevao Willian kuumia misuli ya paja, lakini hakuweza kubadili matokeo.
Baada ya mechi, Garnacho alionekana kubezwa na mchezaji mwenzake wa zamani, Luke Shaw, kupitia mitandao ya kijamii, alipochapisha picha ya tukio akimwangusha chini. Wachezaji wengine wa Man United walionekana kushangilia kejeli hiyo akiwemo Bruno Fernandes aliyeshiriki kwa kutuma kiemoji fulani cha furaha.
Hali hiyo inatia chachu kwa Garnacho ambaye pia alikaribia kuchukuliwa hatua na Chelsea baada ya vitendo vya ajabu alivyofanya kupitia mtandao wa TikTok ikiwa ni pamoja na kufuta maudhui yanayohusiana na Chelsea na kuposti video zake za zamani alipokuwa United.
Garnacho na wenzake walikuwa mzigoni jana dhidi ya Brighton ambao walitoka sare ya mabao 2-2 na Tottenham Hotspur wikiendi iliyopita.
Huo ulikuwa mchezo muhimu kwa Chelsea ambao kabla ya mechi hiyo walikuwa pointi saba nyuma ya Liverpool walio nafasi ya tano, ikiwa ni nafasi ya mwisho ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya zikiwa zimesalia mechi tano msimu huu ili kumalizika.