Man United yaichapa Arsenal kwao
Muktasari:
- Bao la kujifunga la Lisandro Martinez liliipa Arsenal uongozi, lakini Martin Zubimendi alifanya makosa ya kupiga pasi ya nyuma iliyonaswa na Bryan Mbeumo, ambaye alimchambua kipa David Raya na kuisawazishia Man United.
LONDON, ENGLAND: SHUTI la ajabu la Matheus Cunha lilitosha kuizima Arsenal kwao uwanjani Emirates wakati Manchester United ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumapili.
Bao la kujifunga la Lisandro Martinez liliipa Arsenal uongozi, lakini Martin Zubimendi alifanya makosa ya kupiga pasi ya nyuma iliyonaswa na Bryan Mbeumo, ambaye alimchambua kipa David Raya na kuisawazishia Man United.
Patrick Dorgu alifunga bao la ufundi mwingi baada ya kugongeana pasi na nahodha wa Man United, Bruno Fernandes.
Bao hilo lilimshtua Mikel Artata na kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwa mpigo, akiwamo Mikel Merino, aliyeisawazishia Arsenal baada ya kutokea piga nikupige golini kwa Man United kufuatia mpira wa kona.
Wakati Arsenal ikiamini walau itapata sare katika mchezo huo, lakini kumbe Cunha alikuwa na jambo lake, akipiga shuti matata nje ya boksi kufunga bao la tatu na la ushindi kwa Man United na kuleta shangwe kubwa.
Ushindi huo unaifanya Man United kutinga kwenye Top Four, huku Arsenal ikishuhudia pengo lake la pointi kileleni likipungua na kubaki nne baada ya Manchester City na Aston Villa kushinda mechi zao.