Man United wakali wa pira mipasi mirefu
Muktasari:
- Kocha wa Liverpool, Arne Slot alilalamikia staili hiyo ya uchezaji ya wapinzani wake baada ya kikosi chake hicho kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 uwanjani Anfield kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumapili iliyopita.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Manchester United ndiyo wafalme wa mipira mirefu kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot alilalamikia staili hiyo ya uchezaji ya wapinzani wake baada ya kikosi chake hicho kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 uwanjani Anfield kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumapili iliyopita.
Wakati Mdachi huyo, Slot akilalamikia hilo na kuonekana kama anajitetea tu baada ya timu yake kuchapwa, lakini takwimu zinaonyesha kuna ukweli kwenye hilo.
Slot, 47, alisema: “Kama mngeniambia kabla ya mechi tutakwenda kukabiliana na timu inayokabia chini na kupiga mipira mingi mirefu, hilo tungetusaidia kutengeza nafasi nyingi na tusingepoteza mchezo. Lakini, hilo ndilo lililotokea. Tulikuwa na nafasi nyingi za kufunga zaidi ya bao moja, lakini tukaruhusu mabao mawili na moja ya mabao hayo lilikuwa la mpira wa kutenga.”
Man United imepiga pasi 466 za mipira mirefu msimu huu na kwa mujibu wa Opta, hakuna timu nyingine iliyowahi kufanya hivyo.
Kikosi hicho cha Man United kinachonolewa na Mreno Ruben Amorim imeizidi kidogo sana, pasi mbili tu, Wolves, ambapo wamepiga mipira mirefu 464, huku ikiziacha mbali sana Liverpool, Arsenal na Manchester City.
Man City ya Pep Guardiola ndiyo timu iliyopiga pasi ndefu chache zaidi, 307, huku Arsenal ikipiga 350, Liverpool imepiga 366 na Tottenham Hotspur imepiga mipira mirefu 377.
Kocha Amorim, 40, hakuficha kitu kabla ya mechi ya Liverpool, aliposema: “Tuna wachezaji wengi sana wenye nguvu pale mbele. Kama tutashinda mipira inayozagaa baada ya pasi ndefu, tunaweza kujenga mashambulizi kuanzia hapo na kuwa na nafasi ya kufunga.
“Tunahitaji kuwa wasumbufu dhidi ya Liverpool. Lazima tuwe tayari kwa ajili ya mechi. Kipa Senne Lammens anapiga miguu yote. Hivyo ni ngumu kwa wapinzani kumpa presha kipa kutoka upande mmoja. Anapaswa kuwa tayari kwa hilo.”
Kipa mpya wa Man United, Lammens ameleta tofauti kubwa tangu alipotua kwenye kikosi hicho cha Old Trafford kuchukua mikoba ya Altay Bayindir.
Lammens, 23, katika mechi ya Liverpool alipiga mipira mirefu 46, huku tisa tu ndiyo iliyofika kwa walengwa, huku Man United ilikuwa makini sana katika kugombea mipira inayozaa baada ya mipira mirefu. Kipa huyo Mbelgiji alifanya hivyo kwenye mechi yake ya kwanza aliyocheza dhidi ya Sunderland na alipiga pasi ndefu 44 na 17 zilikuwa sahihi.
Kabla ya mchezo wa Jumapili, Man United ilikuwa haijawahi kushinda Anfield tangu 2016, lakini mbinu za Ruben Amorim zilileta matunda kwenye mchezo huo dhidi ya Liverpool.
Katika mchezo huo wa Anfield, Man United ilifunga mabao yake kupitia kwa Bryan Mbeumo na Harry Maguire, wakati Liverpool ilifunga bao lake la kujifariji la Cody Gakpo.
WAKALI WA PASI NDEFU KWENYE LIGI KUU ENGLAND MSIMU WA 2025-26
1.Man United - 466
2.Wolves - 464
3.Everton - 449
4.Bournemouth - 444
5.Burnley - 434
6.Crystal Palace - 429
7.Sunderland - 420