Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United vs Arsenal... Piga ua hawatoki

Piga Pict

Muktasari:

  • Na Liverpool itakuwa na nafasi ya kutanua pengo hilo la  pointi na kufikia 16 endapo itaikamua Southampton katika mchezo wao utakaofanyika Anfield Jumamosi.

LONDON, ENGLAND: MSIMAMO wa Ligi Kuu England unavyosoma, Arsenal imeachwa pointi 13 na vinara Liverpool kwenye msako wao wa kusaka ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Na Liverpool itakuwa na nafasi ya kutanua pengo hilo la  pointi na kufikia 16 endapo itaikamua Southampton katika mchezo wao utakaofanyika Anfield Jumamosi.

Kutokana na hilo, piga ua, Arsenal ambayo itakuwa na mechi mbili mkononi, italazimika kushinda mchezo wao wa Jumapili huko uwanjani Old Trafford dhidi ya wenyeji wao Manchester United ili kuendelea kuwamo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.

Namba za karibuni, zipo upande wa Arsenal kwenda kushinda mechi hiyo Old Trafford. Katika mechi tano za mwisho, Arsenal imeshinda nne na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 10-6. Kwa rekodi za mechi tano zilizopita, Man United ni kibonde kwa Arsenal. Itakuwaje hiyo Jumapili?

Kwenye rekodi za jumla, Man United bado inatunisha misuli kwa Arsenal, baada ya kushinda mechi 26 kati ya 65 ilizokutanisha timu hiyo kwenye Ligi Kuu England, huku Arsenal yenyewe ikishinda 21. Kwenye mechi hizo, Man United imeshinda 18 uwanjani Old Trafford, wakati Arsenal rekodi yao ya kushinda kwenye uwanja huo ni mara tano tu. Je, nani ataongeza rekodi yake?

Arsenal itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na mzuka baada ya kutoka kui-chapa PSV Eindhoven mabao 7-1 ugenini kwenye mchezo wao wa kwanza wa hatua ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano iliyopita, wakati Man United imetoka kutoka sare ya bao 1-1 ugenini mbele ya Real Sociedad kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora kwenye Europa League, usiku wa Alhamisi.

Katika mchezo huo, kila timu itakosa wachezaji wake muhimu, ambako kocha wa Man united, Ruben Amorim hatakuwa na huduma ya wakali wake; Jonny Evans, Mason Mount, Luke Shaw, Lisandro Martinez, Altay Bayindir, Patrick Dorgu, Kobbie Mainoo, Amad Diallo huku wenye hatihati ni Harry Maguire na Manuel Ugarte, wakati upande wa Mikel Arteta kwenye kikosi cha Arsenal, atawakosa Kai Havertz, Gabriel Jesus, Bukayo Saka, Takehiro Tomiyasu na Gabriel Martinelli. Patachimbika.

Kuhusu Liverpool na uwezekano wao wa kutanua pengo la pointi hilo linabebwa na rekodi zao nzuri dhidi ya timu wanayokwenda kukabiliana nayo, Southampton. Kikosi hicho cha kocha Arne Slot kinatoka kushinda 1-0 ugenini dhidi ya PSG kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, rekodi zao za mechi za Ligi Kuu England dhidi ya Southampton, mara 49 ilizokutana, imeshinda 27, mara 15 nyumbani na 12 ugenini, wakati Southampton imeshinda 11, nane nyumbani na tatu ugenini huku mechi 11 zilimalizika kwa sare. Kwa rekodi hizo, uwanja unaonekana kuinama, lakini soka ni mchezo usiotabirika. Ngoja tuone.

Lakini, shughuli pevu kwenye ligi hiyo kwa Jumamosi, itakuwa ya kupanguana kwenye Top Four, ambapo Nottingham Forest itakuwa nyumbani kukipiga na Manchester City. Timu hizo zimetofautiana pointi moja tu kwenye nafasi ya tatu na nne, huku uzuri wa mechi hiyo itapigwa mapema kabisa kujua nani kama Forest itabaki kwenye namba tatu au itapigwa kikumbo kuwapisha mabingwa hao watetezi, Man City.

Rekodi zinasoma kwamba kwenye mechi 11 ilizowahi kuwakutanisha kwenye Ligi Kuu England, mara nne zilimalizika kwa sare, huko Man City imeshinda tano, tatu nyumbani na mbili ugenini, wakati Forest imeshinda mbili na zote ilipocheza nyumbani uwanjani The City Ground. Je, itakuwaje? Pep Guardiola atatulizwa?

Mechi nyingine tamu ya Jumamosi, Brighton - ambayo imewasha moto kwa siku za karibuni, itakuwa nyumbani kukipiga na Fulham, huku Crystal Palace itakuwa Selhurst Park kucheza na Ipswich Town, wakati Unai Emery na chama lake la Aston Villa atakuwa ugenini kukipiga na Brentford, huku David Moyes na wanajeshi wake wa Everton watakwenda kuwakabili Wolves.

Aston Villa na Brentford kwenye Ligi Kuu England zimekutana mara saba tu, ambapo sare ni tatu, huku vijana wa Villa Park wakishinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini, wakati Brentford imeshinda moja tu, ilipocheza kwenye uwanja wao wa Gtech Community.

Fulham kwa Brighton imekuwa ikijipigia tu, ambapo katika mechi tisa zilizopita ilicheza nyumbani na ugenini, sare ni nne, huku Fulham ikishinda tano, nne nyumbani na moja ugenini. Kwa maana hiyo, Brighton haijawahi kushinda mbele ya Fulham kwenye Ligi Kuu England. Palace nayo kwa Ipswich imekuwa ikijipigia tu, kwenye mechi tano zilizopita kwenye ligi, ushindi wa Ipswich ulikuwa sare moja tu, huku ikipoteza kwenye mechi nne, ambapo Palace ilishinda mbili nyumbani na mbili nyingine ugenini, wakati Wolves na Everton zitakazokutana Molineux, ambapo itakuwa mechi yao ya 22 kwenye Ligi Kuu England. Mechi 21 zilizopita, Wolves imeshinda nane, na Everton saba, huku sita zilimalizika kwa sare.

Jumapili, ukiweka kando kipute cha Old Trafford, Chelsea itakuwa mzigoni uwanjani Stamford Bridge kucheza na Leicester City, wakati Tottenham Hotspur nayo itakuwa nyumbani kuikaribisha Bournemouth kwenye moja ya mechi ya kibabe sana.

Leicester City imekuwa na rekodi mbovu msimu huu, itakwenda Stamford Bridge kwa rekodi ya kupoteza mara 19 mbele ya Chelsea katika mechi 35 walizokutana kwenye Ligi Kuu England, huku wao wakishinda sita tu, nne nyumbani na mbili ugenini. Mechi 10 baina yao zilimalizika kwa sare, huku kwenye ushindi wa Chelsea, mara tisa ilikuwa nyumbani na 10 ugenini.

Spurs itakuwa na mechi inayoonekana si ngumu sana kwao kwenye makaratasi kutokana na rekodi zinavyosoma, ambapo kwenye mechi 15 zilizopita, imeshinda 10, sita nyumbani na nne ugenini, huku mechi mbili zilimalizika kwa sare, wakati Bournemouth imeshinda tatu tu, mbili nyumbani na moja ugenini.

Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja kwenye mchakamchaka huo wa Ligi Kuu England, wakati West Ham United itakapokuwa nyumbani kukipiga na Newcastle United. Miamba hiyo imekutana mara 53 kwenye Ligi Kuu England, Newcastle ikishinda 24, mara 13 nyumbani na 11 ugenini, wakati West Ham imeshinda 15, mara tisa nyumbani na sita ugenini, huku mechi 14 zilishuhudia miamba hiyo ikitoka sare. Safari hii itakuwaje?