Man United kuwasilisha ofa mpya kwa Sancho

DORTMUND, ENGLAND. PALE nchini England stori inayozidi kuongelewa kwenye maduka mbalimbali ya kuuzia chakula na vinywaji ni usajili wa winga wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho.

Sancho anatajwa sana kwamba atajiunga na Man United katika dirisha hili baada ya dili lake kushindikana kwenye dakika za mwisho kwenye dirisha lililopita.

Katika dirisha hili Man United ilianza mapema sana kuwasilisha ofa kwa Dortmund ili kuona kama inaweza kupata huduma yake. Lakini baada ya kikao cha muda cha viongozi wa Dortmund walikubaliana kwamba ile Pauni 67 milioni iliyowasilishwa na Man United ilikuwa si chochote kwa staa mkubwa kama Sancho anayewindwa Ulaya nzima hivyo iongozwe.

Baada ya kikao cha mabosi wa Man United imeripotiwa wanatarajia kuwasilisha ofa mpya itakayokaribia Pauni 86 milioni ambayo Dortmund ndio inaihitaji kwa sasa ili kumuuza Sancho.

Katika dirisha lililopita Dortmund ilihitaji kiasi kisichopunga Pauni 108 milioni jambo ambalo lilikwamisha dili kutokana na kiasi hicho cha pesa kuwa maji ya shingo kwa Man United na sasa dili linaonekana kuwa karibu kukamilika kwa sababu bei imeshuka.

Taarifa zinafafanua kwamba dili hilo limebakia kwa Dortmund pekee kwani, wawakilishi wa Man United wameshamalizana na wawakilishi wa Sancho katika maafikiano ya masilahi binafsi ya mchezaji na dili litakuwa ni la miaka mitano kwa sababu hadi masuala ya mishahara wameshakubaliana.

Hata hivyo, watalaamu wa mambo wanasema huenda likatokea lililotokea katika dirisha lililopita kwa jinsi Man United inavyosuasua kwenye kukamilisha dili hilo.

Taarifa kutoka Ujerumani zimefafanua kwamba Dortmund haina mpango wa kuongeza wala kupunguza bei yao ya Pauni 82 milioni kwa Sancho na ikiwa Man United haitatoa haitauziwa.

Bei hiyo hupanda na kufikia Pauni 86 milioni kwa mjumuisho wa pesa nyingine ikiwa ni pamoja na bonasi.

Mwaka jana, Man United ilipewa muda maalumu wa kumaliza dili hilo lakini ikachelewa na mambo yakapinduka. Hali hii inaonekana kuwa huenda ikatokea kwenye dirisha hili kwani Dortmund inahitaji kutambua kama Man United itamsajili Sancho ama laa mpaka kufikia katikati ya mwezi ujao, wakati huohuo Ole Gunnar Solskjaer na timu yake ya usajili wanaonekana kusuasua kwenye kufanya uamuzi.

Katika michuano hii ya Euro inayoendelea, tovuti ya talkSPORT ilipata bahati ya kufanya mahojiano na Sancho ambaye alipoulizwa kuhusu hatma yake kwenye dirisha hili alisema: “Hapana, sina presha. Unajua kila siku tetesi zipo na zinazidi unapokuwa unafanya vizuri, inatakiwa uchunge kile unachofanya ndani ya uwanja kuendelea kukifanya kila siku.

“Kama ukiendelea kucheza vizuri naamini haliwezi kuwa ni tatizo, mimi ninachoamini jambo muhimu ninalotakiwa kulifanya na kulifikiria zaidi ni kucheza mpira na ndio jambo ninalolifanya kwa sasa,

“Nafahamu watu wana maswali mengi, ninachowaambia ni tuangalie lililo mbele yetu ambalo ni michuano ya Euro.”

Sancho ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango kikubwa akiwa na Dortmund tangu ajiunge nayo mwaka 2017, hadi sasa amecheza mechi 104 amefunga mabao 38 na kutoa asisti 51 za Bundesliga wakati kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa amefunga mabao matano akatoa asisti sita kwenye mechi 21.