Man City yatua kwa Florian Wirtz, Bruno Guimaraes
Muktasari:
- Mkataba wa Wirtz mwenye umri wa miaka 21 unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, wakati wa Guimaraes ukimalizika mwaka 2028.
VIUNGO wawili, Florian Wirtz wa Bayer Leverkusen na Bruno Guimaraes, 27, anayeichezea Newcastle United wameingia katika rada za Manchester City inayohitaji kuwasajili dirisha la majira ya baridi mwakani, ili kuboresha eneo lao la kiungo linaloonekana kuwa na mapungufu makubwa msimu huu.
Mkataba wa Wirtz mwenye umri wa miaka 21 unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, wakati wa Guimaraes ukimalizika mwaka 2028.
Guardiola amependekeza kusajiliwa mastaa hawa ili kuboresha eneo lao la kiungo linaloonekana kuwa na mapungufu makubwa tangu kuanza kwa msimu pia uwepo wa majeruhi wa mara kwa mara akiwemo Rodri na Kevin De Bruyne na baadhi ya nyota wake muhimu.
Kutokana na ukubwa wa mikataba ya wachezaji hawa, ripoti zinaeleza kuwa Man City inahitaji kulipa zaidi ya Pauni 150 milioni ili kufanikisha mchakato kuwasajili.
MPANGO wa Arsenal kutaka kumsajili kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi huenda ukafeli baada ya kuibuka kwa ripoti Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola pia anahitaji huduma ya fundi huyo. Zubimendi mwenye umri wa miaka 25, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na msimu huu amecheza mechi 20 za michuano yote, huku kwenye Ligi akihusika na mabao mawili akifunga moja na kuasisti moja katika mechi 16 hadi sasa.
CHELSEA na Liverpool zote zinataka kumsajili beki wa Bournemouth, Milos Kerkez, 21, katika dirisha lijalo lakini mabosi wa Bournemouth wanapambana kwa ajili ya kumbakisha ili aendelee kusalia kwenye viunga hivyo kutokana na mchango wake mkubwa katika timu. Kerkez mwenye umri wa miaka 21, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na msimu huu amecheza mechi 15 za michuano yote na ameonyesha kiwango bora hadi sasa.
REAL Madrid inadaiwa kujitoa katika mpango wa kumsajili beki kisiki wa AC Milan na timu ya taifa ya Ufaransa, Theo Hernandez, 27, kwenye dirisha hili hali inayoweza kuipa Manchester United urahisi wa kufanikisha mchakato huo kwani nayo imekuwa ikimmendea. Theo mwenye umri wa miaka 27, anahusishwa na timu nyingi barani Ulaya ambazo zilihitaji huduma yake tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
RB Leipzig inataka kumsajili mshambuliaji wa Paris St-Germain na Uholanzi, Xavi Simons, 21, ambaye anacheza kwa mkopo katika timu yao lakini wanakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Liverpool ambayo inahitaji kumsajili pia mwisho wa msimu huu. Simos alikuwa akiwindwa na timu nyingi barani Ulaya tangu mwaka jana lakini alikataa ofa nyingi na kuamua kusaini Leipzig kwa mkopo.
KIUNGO wa Manchester United na Denmark, Christian Eriksen, 32, huenda akauzwa dirisha la majira ya baridi mwakani ikiwa itapatikana ofa nono kutoka kwa timu zinazomhitaji. Eriksen sio mmoja wa mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Man United kwa sasa na msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote na kufunga mabao manne na nyingi aliingia akitokea benchi. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu.
EVERTON imepanga kumsajili winga wa Olympique Lyon na Ghana, Ernest Nuamah, 21, katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani. Ernest mwenye umri wa miaka 21, ni mmoja wa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Lyon na msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote na kufunga bao moja.
TOTTENHAM haina mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu straika wa RB Leipzig, Timo Werner anayecheza kwenye kikosi chao kwa mkopo.
Werner mwenye umri wa miaka 28, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Msimu uliopita alicheza mechi 19 za michuano yote na kufunga bao moja.