Man City yaichapa Chelsea, yatinga fainali Kombe la FA

Muktasari:

  • Silva alifuta machungu ya kukosa penalti kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita na hivyo kuipa matumaini Man City ya kunyakua mataji mawili msimu huu baada ya kufika fainali ya Kombe la FA

LONDON, ENGLAND: Bao la kipindi cha pili la Bernardo Silva lilitosha kuipa ushindi Manchester City mbele ya Chelsea katika nusu fainali ya Kombe la FA iliyopigwa uwanjani Wembley leo Jumamosi.

Silva alifuta machungu ya kukosa penalti kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita na hivyo kuipa matumaini Man City ya kunyakua mataji mawili msimu huu baada ya kufika fainali ya Kombe la FA, huku ikisubiri mshindi wa mchezo wa nusu fainali nyingine itakayopigwa kesho Jumamosi kati ya Manchester United na Coventry City.

Kiungo huyo wa Kireno alionyesha utulivu mkubwa na kufunga bao dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho na kumaliza ndoto za Chelsea kubeba taji lolote msimu huu.

Katika mchezo huo, straika wa Chelsea, Nicolas Jackson alikosa nafasi muhimu ya kufunga mapema tu kabla ya Silva kuzitofautisha timu hizo uwanjani kwa bao pekee lililoipa Man City ushindi wa bao 1-0 na kutangulia fainali ya FA.

Chelsea ilishindwa kuweka mpira nyavuni, ikipiga mashuti matano golini, wakati Man City imepiga matatu tu. Mashuti yasiyolenga goli, Man City imepiga matano na Chelsea matatu. Kwenye umiliki wa mpira, Man City ilikuwa na asilimia 63 dhidi ya asilimia 37 za Chelsea, huku vijana wa Pep Guardiola wakipiga krosi 16 na wa Mauricio Pochettino ikipiga krosi 10.