Man City yafukuzia rekodi chafu England
Muktasari:
- Mabingwa hao wa England walikumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Liverpool, Jumapili iliyopita na kuendeleza rekodi yao ya ovyo ya siku za karibuni kwa kushindwa kupata ushindi katika mechi saba mfululizo.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City ipo kwenye hatari ya kufikia rekodi za hovyo za Manchester United baada ya kushindwa kupata ushindi wowote kwenye mechi zao saba za mwisho katika michuano yote.
Mabingwa hao wa England walikumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Liverpool, Jumapili iliyopita na kuendeleza rekodi yao ya ovyo ya siku za karibuni kwa kushindwa kupata ushindi katika mechi saba mfululizo.
Kesho Jumatano usiku, Man City itakuwa nyumbani kukipiga na Nottingham Forest kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, sare au kichapo katika mchezo huo, watakuwa wamefikia rekodi ya hovyo ya mahasimu wao Man United ya kushindwa kupata ushindi kwenye mechi nane.
Man United ilipokuwa chini ya Mdachi Louis van Gaal msimu wa 2015/16, ilicheza mechi nane mfululizo bila ya kupata ushindi.
Hiyo inabaki kuwa rekodi ya muda mrefu zaidi ya kushindwa kupata ushindi kwenye kikosi cha Man United tangu alipoondoka Kocha Sir Alex Ferguson. Katika msimu huo, Man United ilitoka sare na Leicester, West Ham, Chelsea na PSV na kupoteza mbele ya Bournemouth, Norwich, Stoke na Wolfsburg. Ilifunga mabao matano tu na kuruhusu 10 kwenye wavu wao ndani ya siku 33 kati ya Novemba na Desemba.
Mwendo wa ovyo wa Man City umewashuhudia wakitoka sare na Feyenoord na kisha kuchapwa na Bournemouth, Sporting, Brighton, Liverpool na Tottenham mara mbili. Imefunga mabao saba tu, lakini yenyewe ikiruhusu wavu wao kuguswa mara 19 katika mechi hizo.
Man City imeshindwa kupata ushindi kwenye mechi nne mfululizo kwenye Ligi Kuu England. Mara ya mwisho kitu kama hicho kilitokea 2008 wakati kikosi hicho kilipokuwa chini ya makocha Sven Goran-Eriksson na Mark Hughes.
Huko nyuma, Kocha Pep Guardiola hajawahi kucheza mechi nne mfululizo kwenye ligi bila ya kupata ushindi tangu alipoanza ukocha.