Maresca bado yupo sana Chelsea

Muktasari:
- Tovuti ya The Telegraph inaripoti kocha Maresca atabaki Stamford Bridge, bila kujali matokeo ya mechi mbili zilizobaki za msimu huu ambazo ikiwa itapoteza au kutoa sare kuna uwezekano ikaondoshwa katika nafasi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
LONDON, ENGLAND: TAARIFA za ndani kutoka Chelsea zimeweka wazi Kocha wa timu hiyo, Enzo Maresca ataendelea kuwepo msimu ujao hata kama matajiri hao wa Jiji la London watashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tovuti ya The Telegraph inaripoti kocha Maresca atabaki Stamford Bridge, bila kujali matokeo ya mechi mbili zilizobaki za msimu huu ambazo ikiwa itapoteza au kutoa sare kuna uwezekano ikaondoshwa katika nafasi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa sasa Chelsea iko nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England na ushindi katika mechi mbili utafanya klabu hiyo kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao moja kwa moja bila ya kujali matokeo ya timu nyingine.
Hata hivyo, ikiwa itapoteza na Aston Villa ambayo iko nafasi ya sita ikashinda mbili zilizosalia basi itashushwa kwenda nafasi ya sita kwani utofauti wao ni mabao ya kufunga na kufungwa lakini kwa pointi zote zapo sawa zikiwa na 63.
Telegraph, inaeleza Chelsea imekusudia kumpa Maresca ambaye alijiunga nao msimu uliopita kwa mkataba wa miaka mitano, walau misimu miwili kama kocha mkuu kabla ya kufanya tathmini ya utendaji wake.
Hata hivyo, ikiwa itashinda taji la Conference League na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya, uongozi wa Chelsea utachukulia kama msimu wenye mafanikio makubwa.
Ikiwa Chelsea itafeli kufikia lengo lao kuu la kufuzu Ligi ya Mabingwa, itachukuliwa kama ‘kutokuwa na mafanikio’ badala ya ‘ubovu wa kikosi’.
Chelsea itahitimisha msimu wao kwa mechi za Ligi Kuu dhidi ya Manchester United na Nottingham Forest, kabla ya kukutana na Real Betis katika fainali ya Kombe la Conference League.