Mambo 15 gumzo Ligi Kuu England msimu huu

LONDON, ENGLAND. WAKATI Ligi Kuu England ikiwa imesimama kwa muda kupisha mechi za kimataifa, tunaangazia dondoo matata kabisa zinazonogesha ligi hiyo.

Haya hapa mambo yaliyoacha alama kwenye Ligi Kuu England msimu huu wakati Arsenal, Liverpool na Manchester City zikichuana vikali kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo.

Manchester United, Aston Villa na Tottenham Hotspur zenyewe zipo kwenye vita ya kusaka nafasi moja iliyobaki ili kukamilisha Top Four inayoshikilia tiketi ya mwisho ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa utaratibu wa kawaida.

Ngoja tuone itakavyokuwa, wakati kukiwa na vita nyingine pia ya kupambana kubaki kwenye ligi, huku Erling Haaland na wakali wengine kwenye kutikisa nyavu wakichuana kusaka Kiatu cha Dhahabu.

Hizi hapa dondoo tamu kabisa kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu wa 2023-2024.


1. Burnley, Everton, Luton na Sheffield United zote zilipoteza mechi zao tatu za kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ikiwa mara ya kwanza kwenye historia ya ligi hiyo kwa kushuhudia timu nne tofauti zikipoteza mechi tatu za mwanzo wa msimu.

Siku zote ni ngumu kwa timu mpya iliyopanda daraja kuweza kuhimili maisha ya mwanzo kwenye Ligi Kuu England, lakini msimu huu ugumu ulionekana kwa timu zote tatu zilizopanda, huku Everton nayo ikiungana nao kuweka rekodi hiyo matata kabisa ya kuchapwa mechi tatu za mwanzo.


2. Zaidi ya timu tano zimepata nafasi ya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu ikiwamo Liverpool, Arsenal, Manchester City, Newcastle, Brighton, West Ham na Tottenham Hotspur. Kwa msimu uliopita, mambo yalikuwa tofauti, ambapo kulikuwa na timu tatu zilizotawala kilele cha msimamo wa ligi hiyo ambazo ni Arsenal, Spurs na Man City.

Mambo ya msimu huu vita ya kusaka ubingwa imekuwa kali kwelikweli ambapo Arsenal, Liverpool na Man City zimekuwa zikipigana vikumbo kwenye kilele cha msimamo wa ligi.,


3. Hakukuwa na mchezo wowote kati ya 46 ya mwanzo kwenye Ligi Kuu England msimu huu uliomalizika kwa suluhu (0-0). Hiyo ilikuwa rekodi tamu kabisa ya kushuhudia mechi nyingi za ligi ambazo hazikushuhudia mpira ukitinga nyavuni, sawa na ilivyokuwa kwenye msimu wa 2020-21.

Kila mechi ilishuhudia mabao yakitinga kwenye nyavu hadi hapo Bournemouth ilipokipiga na Chelsea uwanjani Vitality, Septemba 17, ambapo timu hizo hazikufungana. Baada ya hapo, sare nyingine za bila kufungana ziliendelea.


4. Hat-trick tatu zilizofungwa Septemba 2 na mastaa Son Heung-min, Erling Haaland na Evan Ferguson, ziliweka rekodi ya kushuhudia hat-trick nyingi zaidi za Ligi Kuu England katika mechi za wikiendi moja.

Mara nyingine kuwahi kutokea tukio kama hilo la hat-trick tatu kufungwa kwenye wikiendi moja ilikuwa Septemba 23, 1995, wakati Alan Shearer, Robbie Fowler na Tony Yeboah wote kila mmoja alipotikisa nyavu mara tatu tatu.


5. Evan Ferguson (miaka 18, siku 318) alikuwa mchezaji wa nne tofauti mwenye umri wa miaka 18 kufunga hat-trick kwenye mechi ya Ligi Kuu England, na akiwa mchezaji kijana zaidi tangu Michael Owen alipofunga dhidi ya Nottingham Forest, Oktoba 1998 (alifunga mabao manne akiwa na umri wa miaka 18 na siku 314).

Chris Bart-Williams na Robbie Fowler ni makinda wengine walioweka rekodi hiyo tamu ya kufunga hat-trick kwenye Ligi Kuu England wakiwa na umri wa miaka 18, sambamba na Ferguson na Owen.


6. Bao la Phil Foden la kwanza alilofunga dhidi ya Nottingham Forest lilitokana na pasi 46, likishika namba mbili kwa kuhusisha pasi nyingi kwenye historia ya Ligi Kuu England tangu msimu wa 2006-07, ambapo Nacer Chadli aliifungia Tottenham katika mechi dhidi ya QPR, Agosti 2014 (pasi 48).

Kwa Man City hilo la Foden ndilo bao lililoshuhudia zikipigwa pasi nyingi kabla ya kufungwa, huku ikidaiwa kwamba linaweza kuwa bao bora la msimu, alipofunga dakika ya saba tu ya mchezo dhidi ya Nottingham Forest.


7. Katika ushindi wao wa mabao 8-0 dhidi ya Sheffield United, Newcastle United ilikuwa timu ya kwanza kushuhudia mabao yote hayo yakifungwa na mastaa wake tofauti katika mchezo huo wa Ligi Kuu England.

Kingine, ushindi huo wa Newcastle wa mabao 8-0 uwanjani Bramall Lane ulikuwa wa kwanza mkubwa zaidi kuwahi kupata kwenye mechi za ugenini katika Ligi Kuu England, huku kilikuwa kipigo kikubwa zaidi kwa Sheffield United kuwahi kukipata kwenye ligi. Katika mechi hiyo mabao yalifungwa na Sean Longstaff, Dan Burn, Sven Botman, Callum Wilson, Anthony Gordon, Miguel Almirón, Bruno Guimarães na Alexander Isak.


8. Kocha wa Crystal Palace, Roy Hodgson alikuwa kocha wa kwanza kucheza mechi tano bila ya kupoteza uwanjani Old Trafford katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England (ameshinda 3, sare 2).

Je, kuna kingine Roy Hodgson kikubwa zaidi anapaswa kufanya? Tangu alipofanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Manchester United, Septemba 30, kocha huyo aliyekuwa akiinoa Palace alikuwa wa nane kufikisha mechi 400 kwenye Ligi Kuu England.


9. Liverpool imekuwa timu ya kwanza kuonyeshwa kadi nne nyekundu katika mechi saba za kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Rekodi hiyo mbaya kwa Liverpool, ilionyeshwa kadi nyekundu mbili zaidi ya misimu iliyopita tangu kocha Jurgen Klopp alipoanza kunoa miamba hiyo ya Anfield. Na kadi hizo nyekundu ni kwenye michuano yote.


10. Bao la ushindi la Declan Rice la dakika 90 aliloifungia Arsenal dhidi ya Manchester United lilikuwa la tatu kwa Man United kuruhusu kufungwa katika dakika za majeruhi za kipindi cha pili kwa mwaka 2023 – ambapo mabao mawili yaliyopita kwenye Ligi Kuu England waliyofungwa kwenye dakika ya 90 ilikuwa kati yam waka 1992 na 2022.

Dakika za majeruhi zimekuwa zikishuhudia mabao ya kutosha, huku Man United iliyokuwa chini ya Alex Ferguson ilikuwa maarufu kwa mabao ya aina hiyo, kabla ya wenyewe kuchapwa na Rice msimu huu.


11. Spurs ilikuwa nyuma hadi dakika 98 katika mechi dhidi ya Sheffield United kabla ya kushinda mabao 2-1; ilikuwa ushindi wa kibeba zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England, wakivunja rekodi yao wenyewe, wakati ilipokuwa nyuma hadi dakika 95 kwenye mechi dhidi ya Leicester City, Januari 2022) na kushinda. Bao la Dejan Kulusevksi la dakika 99:53, ndilo lililotajwa kuwa la dakika za mwisho zaidi kuwahi kufungwa kwenye Ligi Kuu England tangu msimu wa 2006-07.


12. Luton Town ilikuwa timu ya pili kupoteza mechi nne za kwanza kwenye Ligi Kuu England baada ya Swindon Town msimu wa 1993-94.

Baadaye mambo yalibadilika na Luton ingaanza kufanya vyema, lakini bado ipo kwenye vita kali ya kuhakikisha inabaki kwenye Ligi Kuu England ili isirudi tena kwenye Championship.


13. Wolves mabao yao matatu ya kwanza msimu huu yalifungwa na wachezaji waliotokea benchi.

Imekuwa timu ya kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu England kushuhudia mabao yao matatu ya mwanzo wa msimu kufungwa na wachezaji wanaotokea benchi.

Na baada ya hapo, timu hiyo ilishindwa kufunga mabao yake kwa wachezaji wa kutokea benchi, jambo linalofanya rekodi yao ya awali kuwa tamu zaidi.

14. Kwa hat-trick aliyofunga dhidi ya Fulham, Erling Haaland alifikisha mabao 50 kwenye Ligi Kuu England na kumfanya afikishe idadi hiyo akiwa amecheza mechi chache zaidi kwenye historia ya ligi hiyo, mechi 39.

Ubora huo umemfanya Haaland kuwa miongoni mwa mastaa matata na tishio kabisa kwenye kutikisa nyavu za Ligi Kuu England, akiweka rekodi ya kufikia mabao 50 kwenye ligi hiyo kwa haraka.


15. Asisti zote tano za kwanza za Darwin Núñez katika mechi alizochezea timu yake ya Liverpool kwenye Ligi Kuu England, zote mabao yalifungwa na Mohamed Salah.

Jambo hilo limetengeneza rekodi ya kibabe kabisa kushuhudia mchezaji mmoja akitoka asisti nyingi kwa mchezaji mmoja na kufunga mabao kwenye Ligi Kuu England.