Mamadou Sakho kaona sasa inatosha, basi
Muktasari:
- Beki huyo wa kati alitangaza habari hiyo mbele ya umati mkubwa wa mashabiki katika Uwanja wa Parc des Princes kabla ya Paris Saint-Germain kupoteza mchezo wa Kombe la Ufaransa dhidi ya wapinzani wao wa jijini, Paris FC.
PARIS, UFARANSA: BEKI wa zamani wa Liverpool, Mamadou Sakho, ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 35.
Beki huyo wa kati alitangaza habari hiyo mbele ya umati mkubwa wa mashabiki katika Uwanja wa Parc des Princes kabla ya Paris Saint-Germain kupoteza mchezo wa Kombe la Ufaransa dhidi ya wapinzani wao wa jijini, Paris FC.
Sakho, akiwa na hisia kali, ambaye alianza soka lake na Paris FC, aliwaambia mashabiki: “Hii ni furaha kubwa sana kurejea kwenye hapa nikiwa mbele ya umati wa kipekee namna hii. Uwanja bado ni mzuri kama zamani. Nina kumbukumbu nzuri sana hapa.
“Nilitaka kuwajulisha kuhusu mama yangu, kwa sababu bila yeye, simulizi ya maisha yangu ingekuwa tofauti. Heshima kubwa kwa mama wote duniani. Nawashukuru nyote na ninatangaza rasmi kustaafu soka. Asante kwa Parc des Princes na Paris FC, ambao bila wao PSG isingekuwa sehemu ya safari yangu.”
Mashabiki walimiminika kutoa pongezi kupitia mitandao ya kijamii, mmoja akiandika: “Aliibeba Liverpool kuanzia 2013 hadi 2016, mchezaji mkubwa.”
Mwingine aliongeza: “Shujaa anaweka silaha chini mahali palipo na maana zaidi. Salamu, Sakho.”
Mshabiki mwingine amesema: “Taaluma ya kihistoria, Sakho. Asante kwa kila ulichotoa uwanjani. Mparisi halisi kabisa.”
Sakho alicheza mechi 201 akiwa na PSG kabla ya kujiunga na Liverpool mwaka 2013. Aliichezea Liverpool mara 80 kabla ya kukaa kwa miaka minne katika klabu ya Crystal Palace. Alihitimisha taaluma yake kwa vipindi vya kucheza Montpellier na klabu ya Georgia, Kutaisi.
Sakho pia aliichezea timu ya taifa ya Ufaransa mara 29 kati ya mwaka 2010 na 2018.