Majeruhi Arsenal, Arteta anazidi kuvurugwa
Muktasari:
- Vinara hao wa Ligi Kuu England walikuwa na matumaini ya kuendeleza rekodi ya ushindi ya asilimia 100 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipomenyana na Club Brugge ugenini, lakini ilipata pigo baada ya kinda wao matata kabisa, Max Dowman, 15, kupata maumivu siriazi ya enka.
LONDON, ENGLAND: MIKEL Arteta amesema Arsenal ipo kwenye hali ya hatari kutokana na kuandamwa na majeruhi mfululizo kikosini.
Vinara hao wa Ligi Kuu England walikuwa na matumaini ya kuendeleza rekodi ya ushindi ya asilimia 100 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipomenyana na Club Brugge ugenini, lakini ilipata pigo baada ya kinda wao matata kabisa, Max Dowman, 15, kupata maumivu siriazi ya enka.
Dowman, ambaye amechezea kikosi cha kwanza mara tano msimu huu, alipata tatizo hilo wakati alipoitumikia Arsenal ya chini ya Under - 21, Jumamosi iliyopita, wakati kiungo Declan Rice naye alishindwa kusafiri na timu kwa kuwa mgonjwa.
Leandro Trossard na William Saliba nao walibaki England kutokana na kuwa na maumivu. Alipoulizwa kama ni kuzidisha mazoezi ndicho chanzo, Arteta alisema: “Hapana, kwa sababu hatuna muda wa kutosha kufanya mazoezi vizuri. Mazoezi hayapo kwa sababu tunakosa wachezaji wetu, unawapa mzigo wachezaji wengine na hilo ndilo lina madhara yake.
“Declan anaumwa baada ya mechi ya Aston Villa, hivyo hatukusafiri naye. William bado hayupo na Leo (Trossard) pia alipata majeraha mengine. Nimempoteza Big Gabi (Gabriel Magalhaes) na tuna wengine ambao wanaweza kucheza dakika chache sana Richy (Riccardo Calafiori).”
Kutokana na kuumia kwa Dowman, mshambuliaji Gabriel Jesus sasa ameingizwa kwenye kikosi cha Uefa na alikuwapo benchini katika mechi hiyo ya Ubelgiji ya usiku wa Jumatano. Piero Hincapie na Gabriel hawatarudi uwanjani hadi mwezi ujao, wakati Kai Havertz naye alipata tatizo la goti wakati aliporudi mazoezini. Kocha Arteta aliingia kwenye mechi hiyo akiamini Arsenal atarudi kwenye ubora wake wa ushindi baada ya kuchapwa 2-1 na Aston Villa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika wikiendi iliyopita.