Maisha ya upinzani mkali wa Roy Keane na Arsenal

LONDON, ENGLAND. UPINZANI wa Arsenal na Manchester United miaka ya nyuma ulikuwa na idadi kubwa ya watu wanaoongoza, huku Roy Keane akiwa miongoni mwao.

Nahodha huyo wa zamani wa United, ambaye inadaiwa alishambuliwa na shabiki baada ya klabu yake ya zamani kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Arsenal wikiendi iliiyopita kwenye Uwanja wa Emirates, Keane aliwahi kuwa kinara katika mapambano mengi dhidi ya timu hiyo yenye maskani yake London kipindi hicho na matokeo yalikuwa ya aina yake.

Uhusiano mbovu wa Keane na Arsenal uliendelea hata baada ya kustaafu, huku mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ireland akiwapigia simu Gunners mara kwa mara akiwa kwenye majukumu yake ya uchambuzi kwa lengo la kuwakejeli.


Awapiga mbili za kibabe

Baada ya kubeba mataji matatu mwaka 1999, licha ya kukosa mechi ya fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya, Keane alipewa jukumu la kuiongoza Man United katika mbio za kubeba ubingwa wa ligi na jaribio la kwanza ilikuwa dhidi ya Arsenal.

Katika mchezo huo, Freddie Ljungberg alifunga bao la kwanza kabla ya Keane kusawazisha, baadaye Keane alipokea krosi iliyotokana na jitihada za Ryan Giggs na kuingia eneo la hatari kuwekea pasi na Andrew Cole kabla ya kufunga bao la pili. Man United ikabeba ubingwa wa ligi kwa tofauti ya pointi 18 dhidi ya Arsenal kwenye msimamo.


Aongoza ushindi wa bao nyingi

Nahodha huyo aliongoza Man United katika ushindi wa mechi nyingi kubwa za Ligi Kuu England. Februari mwaka 2001 United iliibamiza Arsenal mabao 6-1 katika uwanja wa Old Trafford Keane akiwemo.

Kabla ya mechi hiyo Arsenal ilishinda mechi tatu mfululizo bila ya kuruhusu bao, lakini katika mchezo huo dhidi ya Man United, Arsenal ilijikuta nyuma kwa mabao matatu yakiwekwa kimiani na Dwight Yorke dakika 22 ya mtanange huo huku Keane akiongoza kwa kutoa pasi, na Thierry Henry akifunga bao kwa upande wa Arsenal.

Keane mwenyewe alifunga bao la nne katika ushindi wa mabao sita, Man United ikibeba ubingwa wa ligi kwa mara nyingine.


Hasira kwa Arsenal

Mojawapo ya matukio makubwa katika mechi za United na Arsenal lilikuja msimu wa 2003-04, ambao Arsenal iliumaliza bila ya kupoteza mchezo. Lakini rekodi hiyo ilikaribia kuharibiwa dhidi ya United, ambayo ilipewa penalti ya dakika ya mwisho iliyowakera sana Gunners. Ruud van Nistelrooy alikosa penalti hiyo, mechi ikaisha 0-0. Beki wa Arsenal, Martin Keown alimvaa Van Nistelrooy, lakini Keane alijiweka kando katika vurugu za mchezo huo wa mwaka 2003.

Kutokuwapo kwa Keane katika vurugu hizo kuliwashangaza wengi na alipohojiwa kupitia kituo cha televisheni BBC alijibu: “Nilikuwa na chuki nyingi kwa Arsenal. Sikufikiria neno jingine wakati najiandaa kwa ajili ya mechi dhidi yao. Sikumbuki kama kuna mchezaji yeyote wa Arsenal niliyewahi kumkubali. Arsenal ilileta utofauti mkubwa ndani yangu.”


Ugomvi na Patrick Vieira

Keane alikuwa na mgogoro na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira. Mara nyingi walikuwa wakitibuana uwanjani, lakini huwezi kufananisha ugomvi wao wakati wanaingia uwanjani timu zao zilipomenyana mwaka 2005.

“Nilikuwa nasikia sauti ya Vieira akimuita ‘Neville! Neville! (Mchezaji mwingine wa Man United) akidai hatapata nafasi ya kuwakaba wachezaji wao. 

Baada ya hapo Keane alimfuata Vieira kabla ya kurushiwa chupa ya maji hapo ndipo ugomvi mkubwa ulipoibuka. Kufuatia ugomvi wa Keane na Vieira, Man United iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 baadaye msimu ulipomalizika.


Upinzani unaendelea

Licha ya kustaafu soka chuki yake dhidi ya Arsenal iliendelea, Keane hakuficha chuki zake kuhusu matukio yaliyowahi kutokea kila anapocheza dhidi ya Arsenal.

Keane alisema: “Hivyo ndio inatakiwa unapocheza dhidi ya timu kubwa ambao ni wapinzani, nilipocheza dhidi ya Vieira ilikuwa vita kwa sababu unajaribu kuisaidia timu katika mbio za ubingwa.

“Tulicheza nafasi zinazofanana kwa hiyo ushindani ni mkubwa sana. Hivyo ndio ilikuwa wakati tunacheza soka, mchezaji anapambana kushinda katika mechi kubwa ilikua hatari sana.”


Keane na ubingwa wa Arsenal

Baada ya kushuhudia Arsenal ikikosa ubingwa wa ligi msimu uliopita, Keane aliulizwa kabla ya msimu kuanza kama Arsenal itarudi kwa nguvu baada ya kukosa ubingwa alijibu: “Tusubiri kuona kama Arsenal itakuwa na ushindani, kadri wanavyozidi kwenda mambo yanazidi kuwa magumu. Sidhani kama watabeba ubingwa msimu huu. Hata kama walimaliza nafasi ya pili msimu uliopita, wamesajili wachezaji wapya, haimaanishi kama watafika mbali. Bado wanajifunza kutokana na makosa.”