Mainoo asaini dili la mkwanja mnono Man United
Muktasari:
- Kiungo huyo, ambaye alikuwa akilipwa Pauni 25,000 kwa wiki hivi sasa atalipwa takribani Pauni 120,000 kwa wiki. Kiasi hicho kinaweza kufikia Pauni 150,000 kwa wiki kupitia bonasi.
MANCHESTER, ENGLAND: Nyota wa Manchester United, Kobbie Mainoo amepata nyongeza mara sita ya mshahara baada ya kusaini mkataba mpya wa kubaki katika kikosi hicho hadi mwaka 2031.
Kiungo huyo, ambaye alikuwa akilipwa Pauni 25,000 kwa wiki hivi sasa atalipwa takribani Pauni 120,000 kwa wiki. Kiasi hicho kinaweza kufikia Pauni 150,000 kwa wiki kupitia bonasi.
Mkataba mpya wa Mainoo unaonyesha mabadiliko makubwa katika maisha yake ya soka ndani ya Old Trafford, ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alikuwa nje ya mipango chini ya aliyekuwa kocha wa United, Ruben Amorim.
Mechi yake pekee ya kuanza katika kikosi cha kwanza msimu huu chini ya Amorim ilikuwa wakati United walipotolewa kwa aibu kwenye Kombe la Carabao na timu ya Grimsby Town, Agosti, mwaka jana.
Kupungua kwa nafasi yake kikosini kulizua tetesi kwamba angeweza kuondoka mwezi Januari, huku Bayern Munich na Napoli zikitajwa kumtaka, lakini hali hiyo ilikuwa tofauti kabisa na mafanikio yake, kwani ndiye aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Manchester City kwenye fainali ya FA 2024.
Hata hivyo, viongozi wa United waliamua kumbakiza katika dirisha la usajili la Januari, uamuzi ulioonekana kuwa sahihi baada ya Amorim kufukuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na Michael Carrick hadi mwisho wa msimu wa 2025/26.
Chini ya Carrick, Mainoo ameanza michezo yote 12 ya ligi aliyokuwa tayari kucheza na mechi pekee aliyokosa ilikuwa ile ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Leeds United, Aprili 13, alipokuwa majeruhi. Lakini alirejea moja kwa moja kwenye kikosi katika mchezo uliofuata ambapo United ilishinda 1-0 dhidi ya Chelsea.
Baada ya ushindi huo Carrick alimsifu Mainoo akisema ilikuwa moja ya mechi zake bora tangu arejee kuongoza benchi la ufundi la kikosi hicho na kwamba Mainoo alionyesha utulivu, uimara na ubora hata katika mazingira magumu, akipambana vikali na staa wa Chelsea, Cole Palmer.
Tayari kiwango chake bora kimemfanya arejee katika kikosi cha England ambapo aliitwa kwa mechi mbili za kirafiki dhidi ya Uruguay na Japan. Aliingia kama mchezaji wa akiba kwa dakika 21 dhidi ya Uruguay, na alianza katika mchezo waliopoteza 2-1 dhidi ya Japan.