Maguire kupewa mkataba, Carrick akihusika
Muktasari:
- Mkataba wa sasa wa Maguire Old Trafford unamalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini Carrick ameonyesha kuridhishwa na mchango wake ndani na nje ya uwanja.
KOCHA wa muda wa Manchester United, Michael Carrick, anadaiwa kupendekeza beki wa timu hiyo na England, Harry Maguire, 32, kupewa mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia.
Mkataba wa sasa wa Maguire Old Trafford unamalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini Carrick ameonyesha kuridhishwa na mchango wake ndani na nje ya uwanja.
Uamuzi wa mwisho ikiwa ataendelea kuwepo au la utafikiwa mwishoni mwa msimu. Hadi sasa Maguire ambaye alijiunga na Man United 2019, ni miongoni mwa mastaa waliodumu katika kikosi hicho kwa muda mrefu na Carrick ambaye pia anadaiwa kuwa huenda akapewa nafasi ya kuwa kocha wa kudumu wa Mashetani Wekundu anamhitaji utokana na uzoefu wake.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Maguire aliyekuwa na panda shuka nyingi chini ya kocha aliyepita Ruben Amorim, anaonekana kupata nafasi zaidi chini ya Michael Carrick na ameonyesha kiwango bora ambacho kimemuweka katika nafasi nzuri ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England ambacho kitashiriki michuano ya Kombe la Dunia, mwaka huu.
Curtis Jones
INTER Milan imepanga kurejea tena mezani kufanya mazungumzo na Liverpool kwa ajili ya kumsajili kiungo, Curtis Jones, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kufeli kumpata dirisha lililopita.
Jones yuko karibu kuingia mwaka wake wa mwisho wa mkataba wake katika viunga vya Anfield, jambo linalowapa Inter nafasi ya kujaribu dili hilo wakiamini watampata kwa bei nafuu. Klabu hiyo ya Italia inataka huduma yake ili kuboresha eneo la kiungo ambalo limekuwa na changamoto nyingi msimu huu.
James Trafford
ASTON Villa inadaiwa kuongoza katika mbio za kumsajili kipa wa Manchester City, James Trafford, 23, katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi. Mbali na Villa, Leeds United, Newcastle United, Tottenham Hotspur na West Ham United nazo zinafuatilia kwa karibu hali ya kipa huyo wa timu ya taifa ya England.
Inaelezwa kuwa Manchester City wako tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya staa huyo ikiwa ni kwa mkopo au mauzo ya moja kwa moja kwani bado inahitaji.
Antoine Griezmann
ATLETICO Madrid, imedai haina uhakika juu ya mustakabali wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Antoine Griezmann, 34.
Timu hiyo inadai haijui nini kitatokea kuhusu nyota huyo, ambaye amekuwa akihusishwa kuhamia Orlando City ya Marekani. Griezmann bado ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Atletico, lakini umri wake ni miongoni mwa sababu zinazoishawishi zaidi Atletico kukubali ofa iliyowekwa mezani na kumuuza.
Julian Alvarez
BARCELONA inadai kwamba hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kuhusu kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Argentina, Julian Alvarez mwenye umri wa miaka, 26.
Timu hiyo imesisitiza kuwa kwa sasa haijafanya mawasiliano rasmi wala yasiyo rasmi kwa ajili ya dili la Alvarez ambaye pia amekuwa akihusishwa na Arsenal. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2030. Nyota huyo amekuwa moto tangu atue Hispania.
Alisson Becker
LIVERPOOL haina mpango wa kumuuza kipa wake wa kimataifa wa Brazil, Alisson Becker, 33, katika dirisha la usajili wa majira ya kiangazi yajayo. Mabosi wa Liverpool wamefikia hatua hiyo licha ya klabu ya Juventus kutoka Italia kuonyesha nia ya kumsajili kipa huyo mwenye uzoefu mkubwa. Inaelezwa kwamba Liverpool bado inamchukulia Alisson kama nguzo muhimu ya kikosi chake na haina mpango wa kumuachia kwa sasa.
Tino Livramento
BEKI wa Newcastle United, Tino Livramento, 23, huenda akafikiria kuondoka katika dirisha la usajili wa majira ya kiangazi iwapo atapewa ofa na klabu kubwa Ulaya.
Livramento, ambaye pia amewahi kuitumikia timu ya taifa ya England, amekuwa akihusishwa na vigogo wa Ligi Kuu England, Manchester City. Inaelezwa kuwa mustakabali wake utategemea na ukubwa wa ofa itakayowasilishwa.
Cole Palmer
CHELSEA imeweka wazi haitaingia katika mchakato wa kuuza nyota tegemeo akiwemo winga wa kimataifa wa England, Cole Palmer, 23, licha ya kupata hasara katika msimu wa 2024–25.
Viongozi wa Chelsea wanaamini hali ya sasa ya kifedha inaweza kudhibitiwa bila kuvunja kikosi na wanaona Palmer ambaye alikuwa akiwindwa na Manchester United ni sehemu muhimu ya mradi wao wa muda mrefu wa klabu.