Barca rasmi mezani na Man United dili la Rashford
Muktasari:
- Hata hivyo, Barca inahitaji kupunguziwa bei kutoka Pauni 26 milioni ambazo zinatakiwa ili kumpata Rashford mwenye umri wa miaka 28.
BARCELONA inatarajia kuanza rasmi mazungumzo na Manchester United kuhusiana na uwezekano wa kumsainisha jumla mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford ambaye anaitumikia kwa mkopo.
Hata hivyo, Barca inahitaji kupunguziwa bei kutoka Pauni 26 milioni ambazo zinatakiwa ili kumpata Rashford mwenye umri wa miaka 28.
Licha ya Man United kusisitiza kwamba staa huyo hatauzwa chini ya kiasi cha pesa kilichoandikwa katika mkataba wake, Rashford mwenyewe anatamani kubaki Barcelona kwani anajisikia furaha katika viunga hivyo.
Mkataba wa staa huyo na Manchester United unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028 na ikiwa itashindwa kuishawishi Manchester United kupunguza bei, basi Barcelona inafikiria kuomba tena kumsajili kwa mkopo nyota huyo wa kimataifa wa England ambaye ameonekana kuingia haraka katika mfumo wa kocha Hans Flick.
Mbali ya kuomba kupunguziwa bei, Barca pia imemtaka Rashford mwenyewe kuwa tayari kupokea mshahara wa chini tofauti na ule anaoupokea kwa sasa ikiwa anataka kusajiliwa kwa mkataba wa moja kwa moja.
Morgan Gibbs-White
MANCHESTER United inataka kuwasajili mastaa wawili wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White, 26, na Elliot Anderson, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini inakutana na ushindani mkali kutoka kwa majirani zao, Manchester City ambao pia wanazitaka huduma za mastaa hao. Man United inawataka nyota hao kwa ajili ya kusuka upya safu ya kiungo ambayo msimu ujao itapoteza mastaa muhimu akiwemo Casemiro.
Felix Nmecha
BORUSSIA Dortmund inataka Pauni 61 milioni ili kumuuza kiungo wa kimataifa wa Ujerumani, Felix Nmecha katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Taarifa kutoka tovuti ya Bild zinadai mchezaji huyo anawindwa na Manchester United na Chelsea. Nmecha mwenyewe haonekani kuwa na shauku ya kutaka kulazimisha kuondoka Dortmund, badala yake atasubiri hadi timu hiyo itakapofikia makubaliano na moja kati ya timu zinazomtaka.
Marco Senesi
BARCELONA inadaiwa kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili beki wa kati wa Bournemouth na timu ya taifa ya Argentina, Marcos Senesi, 28, kwa usajili huru dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo mkataba wake unatarajiwa kumalizika. Sensei amekataa kusaini mkataba mpya kusalia Bournemouth na badala yake amewaambia mabosi wa timu hiyo kwamba anataka kuondoka kutafuta changamoto mpya.
Andrea Cambiaso
MANCHESTER City, Liverpool na Real Madrid zinadaiwa kuwa katika vita kali ya kuwania saini ya beki wa pembeni wa Juventus na timu ya taifa ya Italia, Andrea Cambiaso, mwenye umri wa miaka 26. Mabosi wa Juventus hawaonekani kuwa tayari kumuuza staa huyo, lakini mchezaji mwenyewe ameshawaambia kwamba anahitaji kuondoka kwani anaamini ni muda sahihi wa kufanya hivyo.
Guglielmo Vicario
JUVENTUS imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili kipa wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Italia, Guglielmo Vicario, 29, katika dirisha lijalo la majira ya kiangaz. Pia ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa kipa wa Liverpool na Brazil, Alisson Becker. Juventus imekuwa katika mazungumzo na makipa kadhaa tangu dirisha la majira ya baridi mwaka huu kwani hairidhishwi na viwango vya makipa wake wa sasa.
Morgan Rodgers
ASTON Villa inaweza kuwa tayari kumwachia kiungo raia wa England, Morgan Rogers katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini itahitaji kiasi kisichopungua Pauni 100 milioni. Rodgers ambaye anahitajiwa na vigogo wengi Ulaya anaamini huu ni muda sahihi wa kuondoka. Mkataba wa sasa wa nyota huyu mwenye umri wa miaka 23, unatarajiwa kumalizika 2031.
Anthony Gordon
NEWCASTLE United imesisitiza kwamba haina mpango wa kumuuza winga wake wa kimataifa wa England, Anthony Gordon, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa sababu ina matumizi naye. Gordon ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Newcastle na mabosi timu hiyo wanaona kumwachia kwa sasa itakuwa ni kuharibu mipango ya timu ya muda mrefu.