Kompany, Kane waandika historia, Bayern ikitwaa ubingwa Bundesliga

Muktasari:
- Bayern imetwaa ubingwa huo mapema hapo jana, Mei 4, 2025 baada ya Leverkusen kulazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Freiburg matokeo hayo yakiifanya ishindwe kuwafikia vigogo hao wa Bavaria wakati zikiwa zimesalia mechi mbili kumalizika kwa Ligi hiyo.
Bayern Munich imetangazwa kuwa Mabingwa wa Bundesliga msimu huu baada ya Bayern Leverkusen ambayo ilikuwa bingwa mtetezi kushindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Freiburg katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Europa Park.
Bayern imetwaa ubingwa huo mapema hapo jana, Mei 4, 2025 baada ya Leverkusen kulazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Freiburg matokeo hayo yakiifanya ishindwe kuwafikia vigogo hao wa Bavaria wakati zikiwa zimesalia mechi mbili kumalizika kwa Ligi hiyo.
Baada ya matokeo hayo, Bayern ambayo inaongoza Ligi ikiwa na pointi 76, sasa haitaweza kufikiwa na Leverkusen ambayo inashika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nane na hivyo Bayern kutangazwa Mabingwa rasmi msimu huu ikiwa ni kwa mara ya 34 katika Bundesliga.
Hii ni mara ya kwanza kwa kocha Vincent Kompany kushinda taji la Ligi baada ya kuteuliwa kuiongoza timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akitoka kushuka daraja na Burnley. Kompany ameiongoza timu hiyo kushinda mechi 23, akipata sare saba na kupoteza mechi mbili hadi kufikia kutwaa taji hilo.
Mshambuliaji wa kimataifa wa England, Harry Kane, ambaye amejiunga na Bayern msimu uliopita akitokea Tottenham, kwa miaka mingi amekuwa akikosa mataji sasa ameweka historia ya kutwaa Ubingwa wa kwanza wa Ligi huku akiwa amefunga mabao 24 hadi sasa akiongoza orodha ya wafungaji wa Bundesliga.