Mabosi Man United wamfikiria Fletcher kumrithi Amorim
Muktasari:
- Kwa sasa presha inaendelea kumwandama Amorim, ingawa hakuna dalili zozote za kufukuzwa kazi. Hata hivyo, ikiwa matokeo hayataimarika, kuna uwezekano wa kuondolewa katikati ya msimu, na klabu kutafuta kocha wa muda.
DARREN Fletcher ameingia kwenye mbio za kuwa kocha wa muda wa Manchester United endapo Ruben Amorim atafutwa kazi.
Kwa sasa presha inaendelea kumwandama Amorim, ingawa hakuna dalili zozote za kufukuzwa kazi. Hata hivyo, ikiwa matokeo hayataimarika, kuna uwezekano wa kuondolewa katikati ya msimu, na klabu kutafuta kocha wa muda.
Tofauti na hali ilivyokuwa kwa Erik ten Hag, United haijaandaa orodha ya makocha wa kumrithi Amorim. Aidha, kumfuta kazi kabla ya mwezi Novemba 2025 huenda kukaigharimu klabu hiyo takribani pauni 12 milioni kama fidia.
Katika mazingira hayo, United inaweza kuangalia ndani ya klabu kwa chaguo la muda. Kiungo wa zamani wa Man United Darren Fletcher, ambaye sasa ni kocha wa kikosi cha vijana chini ya miaka 18, anaonekana kama mtu mwenye nafasi kubwa.
Fletcher, mwenye umri wa miaka 41, aliteuliwa kushika nafasi hiyo msimu huu wa kiangazi, huku watoto wake wawili Tyler na Jack Fletcher wakipandishwa hadi kikosi cha vijana chini ya miaka 21.
Akiwa kwenye kituo cha mazoezi cha Carrington, Fletcher amevutia wengi kwa namna anavyofundisha vijana wake, akitoa maelekezo ya kina kwa kuzingatia soka la mashambulizi ya haraka, mawinga wanakimbia kwa kasi, na mabao ya aina mbalimbali yakifungwa.
Kiongozi mmoja wa Man United amenukuliwa akisema wamevutiwa na bidii ya Fletcher, na wanaamini yuko njiani kuwa kocha wa kiwango cha juu.
Hata baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti kufuatia jeraha alilopata kwenye mechi ya magwiji kati ya Man United na Celtic iliyochezwa Septemba 2025, Fletcher alirudi kazini haraka na kuendelea kuiongoza timu yake.
Kikosi chake cha vijana chini ya umri wa miaka 18 kimekuwa kikicheza soka la kuvutia, kikiwa kinapambana kuwania ubingwa mapema msimu huu, licha ya kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi vijana, akiwemo JJ Gabriel mwenye umri wa miaka 14.
Timu ya Fletcher haikuruhusu bao hata moja katika mechi sita za kwanza, kabla ya Manchester City kuwapa kipigo cha kwanza cha msimu cha mabao 4-2.
Makocha wengine wanaotajwa huenda wakachukuwa nafasi ya Amorim ni Oliver Glasner (Crystal Palace), Andoni Iraola (Bournemouth) na Fabian Hürzeler (Brighton).
Aidha, SunSport imeripoti kipekee kuwa Gareth Southgate, aliyekuwa kocha wa England, pia anafikiriwa.
Hata hivyo, Southgate mwenye umri wa miaka 55 inasemekana kuwa na mashaka makubwa kuhusu kuchukua nafasi ya Amorim, akihofia hatapewa muda wa kutosha kufanya mageuzi kwenye timu hiyo kama sehemu ya mpango wa muda mrefu.
Kwa sasa, ikiwa Amorim ataondoka, Darren Fletcher anaonekana kuwa chaguo halisi la muda ambalo linaungwa mkono na wengi ndani ya klabu hiyo.