Mabosi Madrid macho kodo kwa kiungo Enzo
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Hispania imeripotiwa kuhitaji saini ya staa huyo wa Chelsea na ipo tayari kufanya dili la kubadilishana na kiungo Aurelien Tchouameni, ambaye atakwenda zake huko Stamford Bridge.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imepanga kufanya usajili wa kushtua wa kuvamia kwenye kambi ya Chelsea kwenda kunasa saini ya kiungo Enzo Fernandez, imeelezwa.
Miamba hiyo ya Hispania imeripotiwa kuhitaji saini ya staa huyo wa Chelsea na ipo tayari kufanya dili la kubadilishana na kiungo Aurelien Tchouameni, ambaye atakwenda zake huko Stamford Bridge.
Na ripoti za kutoka kwa gazeti la Amerika Kusini la DSports, Madrid imepanga kwenda mzima mzima kwenye huduma ya kumnsa Fernandez kutoka Chelsea.
Staa huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 24, alitua Stamford Bridge, Januari 2023 katika dili la Pauni 106 milioni.
Lakini, hadi sasa bado hajaonyesha kiwango bora sana kinachoendana na thamani ya pesa iliyolipwa kupata saini yake licha ya kudumu kwenye kiwango chake katika mechi 87 alizochezea miamba hiyo ya Stamford Bridge.
Kinachoelezwa ni kwamba Madrid ina matumaini ya kufanya usajili huo kwa kufanya dili la kubadilishana na Tchouameni bila ya ziada ya pesa yoyote.
Tchouameni, 24, amekuwa hapati muda wa kutosha wa kucheza chini ya Carlo Ancelotti msimu huu na kinachoelezwa hafurahishwi na mambo yanavyokwenda kwenye klabu hiyo ya Madrid.
Kiungo huyo aliyeichezea timu ya taifa ya Ufaransa mara 36, ameanzishwa mara 15 tu kwenye mechi za La Liga msimu huu na mara kadhaa amekuwa akitumika kwenye beki ya kati licha ya nafasi anayotaka kucheza ni kiungo. Tchouameni alitua Los Blancos mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 85.3 milioni akitokea AS Monaco. Tangu wakati huo amecheza mechi zaidi ya 100, akishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, La Liga na Klabu Bingwa Dunia.