Mabosi Liverpool wanaamini Mo Salah haondoki

LIVERPOOL, ENGLAND. MABOSI wa Liverpool wanaamini kwamba watashinda vita yao ya kumbakiza supastaa Mohamed Salah huko Anfield.

Winga huyo wa kimataifa wa Misri, Mo Salah, Jumamosi iliyopita alitibuana na kocha Jurgen Klopp wakati anasubiri kuingia uwanjani kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya West Ham United kwenye Ligi Kuu England.

Hata hivyo, ripoti zinadai kwamba mabosi wa Liverpool wanaamini hilo haliwezi kumfanya Mo Salah aondoke kwenye timu yao wakati dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Kinachoelezwa klabu za Saudi Arabia zinatajwa kuwinda huduma ya staa huyo wa zamani wa FC Basel, Chelsea na AS Roma na kuna timu ya Saudi Pro League inaweza kuweka mezani Pauni 100 milioni, ambayo inaweza kupanda na kufikia Pauni 150 milioni ili kumng'oa kutoka Anfield.

Hata hivyo, Mo Salah mwenyewe hajaonyesha dalili yoyote kwamba anataka kuondoka. Kwenye umri wa miaka 31, Mo Salah ni kinara wa mabao kwenye kikosi cha Liverpool msimu huu, akifunga mabao 24 katika mechi 41 msimu huu, huku mabao 17 amefunga kwenye Ligi Kuu England.