Mabingwa Ulaya utamu kunoga
Muktasari:
Michuano hiyo ambayo inachezwa kwenye mtindo wa ligi, utashuhudia timu zita za Ligi Kuu England zikirusha kete zao muhimu kwa kuchuana na wababe wengine wa Ulaya ili kusaka pointi muhimu katika kutafuta fursa ya kuvuka hatua ya awali, kuingia kwenye mchujo na hatimaye ubingwa.
ZURICH, USWISI: MCHAKAMCHAKA wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unarudi upya wiki hii, wakati miamba ya soka itakapotupa kete zao za kwanza katika msako wao wa ubingwa wa mikikimikiki hiyo.
Michuano hiyo ambayo inachezwa kwenye mtindo wa ligi, utashuhudia timu zita za Ligi Kuu England zikirusha kete zao muhimu kwa kuchuana na wababe wengine wa Ulaya ili kusaka pointi muhimu katika kutafuta fursa ya kuvuka hatua ya awali, kuingia kwenye mchujo na hatimaye ubingwa.
Mtindo mpya wa michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, utashuhudia mechi zikichezwa kuanzia leo Jumanne hadi Alhamisi, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma na hatua ya makundi iliyokuwa ikichezwa Jumanne na Jumatano tu, huku Alhamisi ikihusisha michuano Europa League.
Mechi zitakazopigwa Jumanne, itashuhudia kikosi cha Arsenal kitakachoanzia ugenini kwa kumenyana na Athletic Bilbao, wakati wababe wa Uholanzi, PSV watakuwa nyumbani kukipiga na Unions Saint-Gilloise.
Benfica itacheza na Qarabag, huku Juventus ikikabiliwa na kasheshe zito la kumenyana na Borussia Dortmund, wakati mabingwa wa kihistoria, Real Madrid wakionyesha ubabe na Marseille na Tottenham itakuwa nyumbani kukipiga na Wahispaniola, Villarreal.
Jumatano, Olympiacos itakwaruzana na Pafos, wakati Slavia Prague itamaliza ubishi na Bodo/Glimt, huku mabingwa wa zamani, Ajax na Inter Milan wataonyesha kazi huko Amsterdam Arena, Chelsea ikisafiri kwenda Allianz Arena kukipiga na Bayern Munich, huku Liverpool ikiwa Anfield kucheza na Atletico Madrid na mabingwa watetezi, Paris Saint-Germain watakuwa nyumbani Parc des Princes kucheza na Atalanta.
Alhamisi kutakuwa na mechi sita na Club Brugge itakipiga na Monaco, Copenhagen na Bayer Leverkusen huku Eintracht Frankfurt ikicheza na Galatasary, wakati Manchester City itakuwa uwanjani Etihad kukabiliana na staa wao wa zamani Kevin De Bruyne akiwa na chama lake jipya la Napoli.
Newcastle bila ya huduma ya straika Alexander Isak, aliyetimkia Liverpool itakuwa St James' Park kucheza na Barcelona ya Lamine Yamal, huku Sporting Lisbon ikiwa na shughuli mbele ya Kairat.